Njama ya wabunge kukinga minofu yao
WABUNGE wameanza jaribio la kukinga mabilioni ya fedha wanazosimamia kupitia hazina zinazowafaidi kisiasa kwa kutayarisha mswada wa kuweka hazina hizo mwenye Katiba.
Mswada huo unalenga kuhakikisha kuwa Hazina ya Ustawi wa Maeneo ya Bunge (NG-CDF), Hazina ya Kitaifa kuhusu Usawazishaji (NGAAF) na Hazina ya Kuwafadhili Maseneta Kufuatilia Utendakazi wa Kaunti (SOF) zitambuliwa rasmi na kulindwa na Katiba ya sasa.
Hatua hii kwanza inaonekana kama jaribio la kuokoa NG-CDF kufuatia uamuzi wa Septemba 2024 wa Mahakama Kuu kwamba hazina hiyo ni haramu na isitengewe fedha zozote kufikia Juni 30, 2026.
Pendekezo la kukika hazina hizo katika Katiba liko kwenye Mswada wa Marekebisho ya Katiba ya 2025 uliwasilishwa bungeni Machi 6, 2025 na Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo na mwenzake wa Ainabkoi Samuel Chepkonga.
“Lengo kuu la mswada huu ni kuifanyia Katiba marekebisho ili kuziweka hazina za NG-CDF, NGAAF na SOF kwenye Katiba,” mswada huo unasema.
Hatua hii itazipa hazina hizo tatu msingi wa kikatiba wa kuendesha shughuli yazo kwa kutumia mabilioni ya fedha zinazotengewa kila mwaka, baada ya mahakama kuamua kuwa uwepo wa NG-CDF unakiuka Katiba.
“Kuwekwa kwa NG-CDF kwenye Katiba kutaiwezesha kufadhili majukumu ya serikali ya kitaifa pekee katika maeneobunge inavyohitajika kulingana na Kipengele cha 6 (3) cha Katiba na kuhakikisha wananchi wanashiriki katika utambuaji na utekelezaji wa mipango ya serikali ya kitaifa,” mswada huo unaeleza.
Unaongeza kuwa pesa zitakazotumika na hazina hiyo ni zile zitakazogawiwa serikali ya kitaifa kwa mujibu wa Sheria ya Ugavi wa Mapato.
Wabunge, pia, wanatarajiwa kupitisha sheria itayotoa mwelekeo kuhusu namna pesa zilizotengewa hazina ya NG-CDF zitatumika na jinsi hazina hiyo itakavyoendeshwa baada ya kuwekwa kwenye Katiba.
Septemba 2024, Mahakama Kuu iliamua kuwa hazina ya NG-CDF, ilivyo sasa, inakiuka Katiba. Hazina hiyo imetengewa Sh54.7 bilioni katika mwaka huu wa kifedha unaofikia kikomo Juni 30, 2025.
“NG-CDF na miradi, mipango na shughuli zake zote zitasitishwa mnamo Juni 30, 2026,” Mahakama Kuu ikaamua.
Wabunge wamekuwa wakitumia hazina ya NG-CDF kwa manufaa yao ya kisiasa, kupitia miradi na mipango inayofadhiliwa na pesa za hazina hiyo, hususan basari kwa wanafunzi.
Maseneta, pia, wanataka kusimamia hazina kama hiyo wakisukuma kuanzishwa kwa hazina ya SOF itakayowawezesha wale waliochaguliwa kusimamia mabadilioni ya fedha zitakazotengewa hazina hiyo.
Kulingana na mswada huo, kuanzishwa kwa SOF kutahakikisha Maseneta “wamepata rasilimali na uwezo wa kutekeleza wajibu wao wa kuhakiki utendakazi wa serikali za kaunti.”
Fedha za hazina hiyo zitatengwa kutoka kwa mgao wa fedha kwa Serikali ya Kitaifa ulivyogawanywa kila mwaka na Sheria ya Ugavi wa Mapato, sawa na zile za NG-CDF.
“Kuwekwa kwa SOF katika Katiba kutahakikisha kuwa Seneti inapata rasilimali na nguvu za kuiwezesha kutekeleza majukumu yake ya kuhakiki utendakazi wa serikali za kaunti,” Mswada huo unasema.
Hazina ya NGAAF, ambayo imekuwa ikiendeshwa chini ya usimamizi wa wabunge wawakilishi wa kike, pia inatarajiwa kuhalalishwa kikatiba.
“Hii itaimarisha hatua ambazo serikali kuu inatekeleza kuhakikisha usawazishaji kimaendeleo,” inaeleza mswada huo.
Ripoti kadhaa za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali zimeibua maswali kuhusu matumizi ya mabalioni ya fedha zinazotengewa hazina za NG-CDF na NGAAF, ikiwemo usambazaji wa pesa za basari kwa wanafunzi kutoka familia maskini.
Ripoti hizo zimewahi kuibua visa ambapo pesa hizo zinatumika kwa mambo mengine au zinaporwa.
Tafsiri: CHARLES WASONGA