Habari za Kitaifa

NMG yapata Afisa Mkuu Mtendaji mpya

Na CHARLES WASONGA April 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SHIRIKA la Habari la Nation (NMG), limepata Afisa Mkuu Mtendaji mpya, Bw Geoffrey Odundo ambaye aliingia afisini mnamo Jumanne, Aprili 7, 2025 na kuanza kuchapa kazi rasmi akiahidi kuendeleza ajenda ya mfumo wa kidijitali kupeperusha habari, taarifa na matangazo uliokumbatiwa na Nation.

Bw Odundo aliteuliwa kufuatia kustaafu kwa mtangulizi wake, Stephen Gitagama aliyehudumia NMG katika nyadhifa mbalimbali kwa miaka 17.

Tangu kustaafu kwa Bw Gitagama Agosti 1, 2024, Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Kifedha Richard Tobiko amekuwa akihudumu kama kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika hili kuu la habari katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NMG, Dkt Wilfred Kiboro, alimjulisha Bw Odundo kwa wafanyakazi wa kampuni hii katika mkutano wa kwanza wa mwaka huu Ijumaa, Aprili 4, 2025.

“Ni fahari yangu kupata nafasi ya kuongoza shirika hili kubwa la habari Afrika Mashariki. NMG imekuwa safarini kutekeleza mfumo wa utoaji habari kidijitali. Naamini tunaweza kuendeleza utekelezaji wa ajenda hii ya kiteknolojia kutoa habari sahihi, na kwa haraka kwa wateja wetu,” akasema Bw Odundo katika hotuba yake ya kwanza kwa wafanyakazi.

Kabla ya kuteuliwa, Bw Odundo, ambaye ni mtaalamu katika masuala ya kifedha, alihudumu kama Mshauri Mtendaji katika kampuni ya kifedha ya kimataifa CPF Group.

Awali, alihudumu kama Afisa Mkuu Mtendaji wa Soko la Hisa la Nairobi (NSE).

Aidha, amewahi kushikilia vyeo vikubwa nchini, ikiwemo Shirika la Biashara ya Hisa ya Kingdom Securities.

Dkt Kiboro alisifia rekodi ya utendakazi ya Bw Odundo katika kampuni ambazo amewahi kuhudumu, akiahidi kuwa wanachama wa bodi na wafanyakazi wa NMG watamuunga mkono.

“Bw Odundo ni afisa wa hadhi ya juu ambaye amewahi kuhudumu katika mashirika ya kifedha na mwenye tajriba ya miaka mingi kama Afisa Mkuu Mtendaji wa Soko la Hisa la Nairobi ambako aliandikisha ufanisi mkubwa kati ya 2015 na 2024.

“Kwa hivyo nina imani kwamba nitakutegemea pakubwa katika kuiwezesha NMG kufikia malengo na ajenda yetu kwa wateja wetu,” Dkt Kiboro akaeleza.

Bw Odundo alitoa hakikisho kuwa atatumia tajriba aliyopata katika mashirika mbalimbali katika sekta ya fedha kuhakikisha kuwa NMG itatekeleza wajibu wake wa kuchochea mabadiliko bora katika jamii.

“Nimewahi kutagusana na vyombo vya habari na kuelewa wajibu wavyo katika nyanja za kiuchumi, kidemokrasia na kijamii katika nchi hii na ulimwengu kwa ujumla. Kwa hivyo, lengo langu ni kuhakikisha NMG inaendelea kushikilia rekodi ya kuwa chanzo cha habari sahihi kwa watu wa matabaka mbalimbali,” akaeleza.