NTSA yasimamisha leseni ya Super Metro
MAMLAKA ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) imesimamisha leseni ya kampuni ya Super Metro Limited hadi kampuni hiyo itakapozingatia kikamilifu kanuni zinazosimamia magari ya huduma za umma za mwaka 2014 na masharti mengine ya kisheria.
Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi, Machi 20, NTSA iliwatahadharisha wananchi dhidi ya kupanda magari yanayomilikiwa na kampuni hiyo ambayo pia ni chama cha akiba na mikopo cha matatu.
“Hii ni kuwajulisha umma kwamba Mamlaka imesimamisha leseni ya Super Metro Limited hadi kampuni itakapozingatia kikamilifu kanuni za magari ya huduma kwa umma za mwaka 2014 na masharti mengine yaliyowekwa,” sehemu ya taarifa hiyo ilisema.
Polisi wa trafiki pia wameagizwa kukamata magari yanayomilikiwa na kampuni hiyo.
Kulingana na NTSA, ilifanya uchambuzi wa kina kuhusu Super Metro na kugundua kuwa kati ya magari yake 523, 15 yalikuwa na vyeti vya ukaguzi vilivyomaliza muda wake, na manane yalikuwa na Leseni za Huduma za Barabara (RSL) ambazo muda wake ulikuwa umemalizika.
NTSA pia iligundua kuwa madereva kadhaa kutoka kampuni hiyo hawana sifa zinazohitajika, jambo ambalo ni hatari kubwa kwa usalama.
Kabla ya kurudishiwa leseni, Super Metro imeagizwa kuwasilisha magari 294 kwa ukaguzi katika Kituo cha Ukaguzi wa Magari cha Likoni.
Kusimamishwa kwa leseni ya kampuni hiyo, kunafuatia mfululizo wa ajali za barabarani zilizohusisha Super Metro na kusababisha vifo kadhaa. Tukio la hivi karibuni lilitokea Machi 12, ambapo kondakta alidaiwa kumsukuma mwanaume kutoka basi likitembea kwa dai la kutolipa nauli.