Nyutu afichua ‘uongo’ wa Ruto, akimfananisha na Herode kwa kulenga viongozi Mlima Kenya
SENETA wa Kaunti ya Murang’a, Joe Nyutu, amemshutumu Rais William Ruto kwa kuwalenga viongozi wanaochipuka Mlima Kenya na kupania kuzima ndoto zao kisiasa.
Huku akimlinganisha Rais Ruto na Mfalme Herode wa Biblia, alimshutumu vikali kwa kuwalenga viongozi wanaochipuka Mlima Kenya akirejelea aliyekuwa naibu rais Gachagua, Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, Maseneta John Methu (Nyandarua), Karung’o Thangwa (Kiambu) na wengineo.
“Njama ya Ruto ni kwamba anataka kuua azma ya kila kiongozi anayechipuka Mlima Kenya. Kila kiongozi anayeonyesha ishara za kuwa kiongozi mlima kiongozi ni sharti aangamizwe,” alisema Seneta Nyutu akihutubia vyombo vya habari Jumanne, Aprili 1, 2025 katika majengo ya bunge.
“Gachagua alipoonyesha kuwa na ujasiri kumpinga Ruto alipoanza kutenga Mlima Kenya na kuangamiza hatima za viongozi kutoka eneo hilo, ilibidi arushwe nje.”
Akirejelea mahojiano yaliyofanyika katika Ikulu Nogo ya Sagana Jumatatu, Machi 31, Seneta Nyutu alipuuzilia mbali madai ya Rais Ruto kuhusu kuwa kielelezo kwa mbunge wa Kiharu na utendakazi duni wa aliyekuwa Waziri Justin Muturi.
“Ni katika skuli ya Ruto pekee ambapo mafunzo ya kielelezo bora hutolewa kwa wanaofutwa kazi. Bw Nyoro anapatiwa mwongozo baada ya kufutwa kazi. Kimani Ichungwa (Kikuyu) na Eric Wamumbi (Mathira) hawapatiwi mwongozo kwa sababu hawajapigwa kalamu. Watakapopigwa kalamu wataanza kupatiwa mwongozo,” alisema.
Bw Nyutu, vilevile, alihoji ni vipi utendakazi duni unapatikana tu miongoni mwa viongozi kutoka Mlima Kenya.
Aidha, alikosoa matamshi ya Ruto katika mahojiano hayo akisema yalikinzana na yalikusudiwa kuwapotosha Wakenya.
Alimsuta Ruto kwa kusema hakuhusika na ufurushaji wa aliyekuwa Naibu Rais na wakati huo vilevile kukiri ndiye aliyepatia bunge idhini ya kumtimua Bw Gachagua.
“Alisimulia taifa kuhusu safari ya mivutano kati yake na Rigathi Gachagua. Alisema wabunge walimwendea mara mbili na kila wakati alisema la kuhusu kumtimua Gachagua. Ina maana ilipofanyika hatimaye, na alithibitisha, walikuwa na baraka kutoka kwake. Alisema walipomwendea mara ya tatu walimweleza ni lazima wangemtimua na akawapa baraka zake,” alisema.
Kuhusu madai kwamba Bw Gachagua alimshurutisha Rais Ruto kumpa Sh10 bilioni ili akimye, Seneta Nyutu alisema kauli ya Bw Ruto ilikinzana na mshauri wake wa kidijitali, Dennis Itumbi, aliyedai awali kwamba Bw Gachagua aliitisha Sh6.4 bilioni.
“Kumekuwa na madai chungunzima. Tunajua kipimo cha ukweli ni ukosefu wa mtiririko wa maelezo. Kama hakuna mtiririko basi inakueleza si ukweli,” alisema.
Alirejelea mahojiano kwenye kipindi cha JKL 2022 ambapo aliyekuwa waziri Raphael Tuju alifichua jinsi Bw Ruto alivyoitisha hela kutoka kwa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa 2013 ili amuunge mkono.
Katika mahojiano hayo, Bw Nyutu alisema, “siku 14 kabla ya uchaguzi mkuu 2013, Bw Ruto aliitisha hela kutoka kwa Bw Uhuru akisema alihitaji pesa ili kuwashawishi watu wake.”
Kulingana na Seneta Nyutu,” Ruto alidhani alichomtendea rais mstaafu ndicho alichokuwa akifanya Gachagua. Kwa sababu inafahamika aliitisha pesa ili amuunge mkono Uhuru Kenyatta.
Kuhusu miradi ya maendeleo, Seneta Nyutu alimshutumu Rais Ruto kwa kudanganya kuhusu ujenzi wa barabara ya Wamunyoro iliyojengwa na Bw Gachagua alipokuwa akihudumu kama mbunge wa Mathira.
“Sote tunajua hiyo barabara ilifunguliwa 2020 na tuna picha za Bw Gachagua alipokuwa akihudumu kama mbunge wakati huo akizindua barabara hiyo.”
Bw Nyutu vilevile alimkosoa Rais kwa kutaja barabara hewa miongoni mwa miradi aliyodai amezindua Murang’a.
“Kinachonitatiza zaidi ni barabara aliyotaja Murang’a ambayo haipo. Hakuna barabara Murang’a inayounganisha Kiharu-Maragua-Kandara jinsi alivyosema. Ninamshauri arejelee tena nakala zake ili athibitishe ikiwa kuna barabara kama hiyo.”
Alifichua hakuna ujenzi wowote ulioanzishwa kuhusu barabara za MauMau Murang’a akisema, “hata inchi moja haijajengwa. Nataka rais katika ziara yake aonyeshe barabara hata moja ya Maumau iliyoanza kujengwa.”