Habari za Kitaifa

Oburu Odinga: Raila alikuwa wembe darasani

Na SAMMY WAWERU October 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

NDUGUYE mkubwa wa Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, Oburu Odinga, amemtaja marehemu Raila kama kaka aliyekuwa mwerevu darasani.

Bw Raila anazikwa leo, Jumapili, Oktoba 19, 2025 nyumbani kwake Bondo, Kaunti ya Siaya, mazishi yanayoongozwa na Rais William Ruto.

Oburu, akimkumbuka, alimuomboleza kakake kama ‘mtoto’ aliyekuwa wembe darasani.

“Ndugu yangu (Raila Odinga) alikuwa mtoto na mwanafunzi mwerevu darasani,” seneta huyo wa Siaya akaambia maelfu ya waombolezaji.

Pia soma: https://taifaleo.nation.co.ke/makala/jamvi-la-siasa/haiyaa-kitendawili-hadi-tibim-raila-azikwa-na-ucheshi-wake/

Bw Raila, ni mhandisi na amewahi kuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Aidha, alikuwa na Shahada ya Uzamili (Master’s degree in mechanical engineering) kutoka Ujerumani.

Seneta Oburu, akimmiminia sifa marehemu Raila, vilevile alisema alikuwa shabiki wa soka.

“Alipenda kandanda sana, na alikuwa patroni wa timu ya Gor Mahia.”

Pia soma: https://taifaleo.nation.co.ke/makala/jamvi-la-siasa/raila-aacha-pengo-kenya-na-afrika/

Bw Raila, ambaye amesifiwa kutokana na mchango wake wa kisiasa nchini haswa kutetea utawala wa vyama vingi 1992 na uhuru wa demokrasia, alifariki mnamo Oktoba 15, 2025 nchini India alikokuwa akipokea matibabu. Aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 80.

Kando na Dkt Ruto, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, naibu wa rais Prof Kithure Kindiki, Mkuu wa Mawaziri, mawaziri, kati ya viongozi wengine wakuu serikali, ni miongoni mwa watu mashuhuri waliohudhuria mazishi ya Bw Raila.

Mazishi hayo, pia, yalihudhuriwa na viongozi wengine kutoka nje ya nchi, akiwemo rais mstaafu Nigeria, Bw Olusegun Obasanjo.

Waziri Mkuu huyo wa zamani, anatarajiwa kusindikwa kwa dhima za kijeshi ambapo mizinga itafyatuliwa na Jeshi la Kenya (KDF).