Habari za Kitaifa

Okanga aomba kesi dhidi ya wapinzani wa Ruto zifutwe

Na RICHARD MUNGUTI August 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NURU Okanga, mfuasi sugu wa kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga,  anaomba Serikali ifutilie mbali kesi zote dhidi ya waliokuwa wanapinga serikali ya Rais William Ruto.

“Kufuatia kuungana kwa ODM na Serikali ya Rais Ruto, Bw Odinga ashinikize kesi walizoshtakiwa wafuasi wake na wanachama wa ODM na muungano wa Azimio zifutiliwe mbali zote,” Okanga aliambia Taifa Leo katika mahakama ya Milimani.

Okanga anayekabiliwa na kesi kadhaa za uchochezi dhidi ya serikali alisema, “Kwa vile upinzani uko pamoja na serikali, itabidi kesi zote dhidi ya wafuasi wa ODM /Azimio zitamatishwe.”

“Sasa vita dhidi ya serikali vimekoma. Upinzani uko serikalini sasa. Tulichokuwa tunapinga serikalini sasa kitarekebishwa,” aliongeza Okanga ambaye pia ni mwanachama wa Bunge la Wananchi.

Mdokezi huyu wa masuala ya kisiasa pia aliomba kesi dhidi ya vibarua wanne wa mwanasiasa Jimi Wanjigi itamatishwe.

“Pia naomba kesi za wote wanaohusishwa na Odinga ikiwa ni pamoja na vibarua wanne wa kiongozi wa chama cha Safina Jimi Wanjigi ifutiliwe mbali,” Okanga alirai.

Jitahada za vibarua hao wanne kupinga kushtakiwa kwa umiliki wa vilipuzi na grunedi ambazo polisi walidai Agosti 8, 2024 ni za Wanjigi, ziliambulia patupu.

Hakimu mwandamizi Rose Ndobi alitupilia mbali ombi la Duncan Odhiambo Otieno, Calvin Odhiambo Odongo, Kennedy Ochieng Asewe na Josiah Augo Otimo la kuharamisha kushtakiwa kwao kwa umiliki wa silaha hatari.

Washtakiwa hao walisema wao ni majeruhi wa malumbano makali kati ya serikali na mwanasiasa Jimi Wanjigi.

Waliomba korti iwatenganishe na masuala ya siasa na kuamuru ‘majitu hawa wa kisiasa’ walumbane pasi kuwashirikisha.

“Washukiwa hawa ni wananchi wa kawaida na vibarua waliokuwa wanafanya kazi kwa Wanjigi polisi walipovamia makazi  ya bwanyenye huyo. Hawajui chochote kuhusu grunedi na vilipuzi hizi wanazoshtakiwa kuwa nazo siku ya maandamano ya Nane Nane mnamo Agosti 8,2024,” Wakili Dkt Owiso Owiso alimweleza Bi Ndobi.

[email protected]