Osoro na Raila wabishana kuhusu mgao wa fedha kwa kaunti
KIRANJA wa Bunge la Kitaifa, Bw Sylvanus Osoro, ametofautiana na kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, kwamba Bunge linalemaza shughuli za kaunti kwa kutopitisha mswada wa ugavi wa mapato ya kaunti katika muda unaofaa.
Bw Osoro alisema matamshi ya Bw Odinga si sahihi kwani wabunge wanafuata sheria ndiposa suala hilo limeundiwa kamati maalum ya wabunge na maseneta kulijadili.
“Bw Odinga kulaumu Bunge hana msingi wowote kwani Bunge la Kitaifa na lile la Seneti lilitofautiana kuhusu kiwango cha fedha za kutengewa kaunti. Ndiyo sababu hadi sasa fedha hizo hazijatumwa mashinani. Bw Odinga na washauri wake hawakufanya uchunguzi wa kina kabla kutoa matamshi hayo,” alieleza Bw Osoro.
Mbunge huyo wa Mugirango Kusini alisema amesikitishwa na matamshi ya Bw Odinga ikizingatiwa kuwa kiongozi huyo alihusika pakubwa kuunda Katiba ya sasa ambayo ni lazima ifuatwe. Hata hivyo, Bw Osoro alieleza kwamba Bunge liliamua kaunti zitengewe Sh380 bilioni kutokana na taarifa tele za ubadhirifu wa fedha katika kaunti.
“Inasikitisha kuona magavana wakitumia vibaya fedha za umma. Kwa mwaka wanapokea pesa zisizopungua Sh500 bilioni lakini mashinani hakuna miradi ya kuendana na fedha hizo. Ndiposa tukaona mgao wa kaunti uwe Sh380 bilioni hadi pale magavana watakapowajibika,” alisisitiza Kiranja huyo.
Vile vile, Osoro alimsuta Bw Raila kwa kuunga mkono wabunge wasipate Hazina ya Kitaifa ya Ustawi wa Maeneobunge (NG-CDF) akisisitiza fedha hizo kidogo zimeleta mabadiliko makubwa mashinani.
“Wabunge hawahusiki na fedha hizo, wao ni kuhakikisha zinatumika vilivyo. Hivyo, viongozi wanaofikiri wabunge hufaidi kutokana na NG-CDF hawasemi ukweli wowote,” akaeleza.
Mnamo Ijumaa, Novemba 15, 2024, Bw Odinga aliunga mkono kauli ya Seneti kwamba serikali za kaunti zitengewe Sh400 bilioni huku akishutumu Bunge la Kitaifa kwa kuhujumu ugatuzi.
Bunge na Seneti kwa sasa zinavutana vikali kuhusu mgao huo kwa serikali zote 47 za kaunti.
Maseneta wanataka kaunti zimegewe Sh400 bilioni huku Bunge likipendekeza Sh380 bilioni.
Mzozo kuhusu salio hilo la Sh20 bilioni umezidi kutokota hata baada ya kuundwa kwa kamati ya pamoja ya patanisho, ambayo wanachama wake 18 wanatoka mabunge hayo mawili kwa usawa.
Bw Odinga alisema inashangaza kwamba Bunge linashinikiza kupunguzwa kwa kitita hicho cha kaunti, akilinganisha shinikizo hizo na kamba inayonyonga serikali za kaunti na kuangamiza ugatuzi pole pole.