PAA yalia inatengwa ndani ya serikali ya Kenya Kwanza
CHAMA cha Pamoja African Alliance, kinachohusishwa na Spika wa Bunge la Seneti Bw Amason Kingi, kimeanza kuhisi kutengwa na serikali ya Kenya Kwanza.Hii ni baada ya muungano kati ya Rais William Ruto na Kinara wa ODM Raila Odinga.
Chama cha ODM kimevuna pakubwa kupitia uteuzi wa wanasiasa wake kwenye baraza la mawaziri akiwemo Bw Hassan Joho (Madini na Uchumi Samawati), Bw John Mbadi (Fedha), Bw Wycliffe Oparanya (Ushirika), na Bw Opiyo Wandayi (Kawi).
Katibu mkuu wa PAA, Bw Kenneth Kazungu, alisema chama hicho ambacho makao yake makuu ni Mombasa hakitamezwa na UDA. Badala yake, alisema watajishughulisha na kusaka wanachama zaidi ili kuongeza idadi yao bungeni katika uchaguzi mkuu ujao.
Kwa sasa chama hicho kina wabunge watatu na wawakilishi wa wadi kadhaa. Akiongea kwenye mkutano katika afisi zao Nyali, Mombasa, Bw Kazungu alisema chama cha PAA kimesalia ‘yatima’ serikalini.
“Wapinzani wetu wanaendelea kuvuna kwenye serikali kwa sababu wako na wabunge wengi. Wanasikizwa zaidi kutuliko sisi ambao tumekuwa ndani tangu serikali hii ilipoingia serikalini. Tuko kwenye hatari. Hatuwezi kupigana na ODM kwa sababu wana idadi kubwa ya wabunge,” alisema Bw Kazungu.
Bw Kazungu ambaye ni mbunge wa Ganze kupitia chama cha PAA alisema ODM inavuna kwenye serikali kuliko chama chochote kwenye serikali hiyo ya muungano.
Alisema chama hicho pia kitagombea kiti cha ubunge Magarini na kumenyana na UDA na ODM.
Bw Kazungu alisema endapo chama hicho kinataka kupata uteuzi serikalini kinafaa kuwa na wabunge wengi.
Alisem PAA ilitia saini mkataba na Rais Ruto ambao ungehakikisha anatatua changamoto za wapwani ikiwemo ukosefu wa ajira, na unyakuzi sugu wa ardhi.
“Lakini hadi wa leo kuna changamoto hazijatatuliwa kama tulivyotarajia. Lakini ni sababu pia sisi hatukutimiza ahadi,” alisema.
Haya yanajiri huku viongozi wa ODM wakiendelea kumshinikiza Rais Ruto kuhakikisha kiti hicho kinasalia katika chama chao.
Kwenye ziara yake hivi majuzi Rais Ruto alisema atahakikisha kuna makubaliano kwenye kinyanganyiro hicho.