Habari za Kitaifa

Pigo kwa Kidero korti ikikataa ombi lake katika kesi ya Sh58 milioni

Na  JOSEPH WANGUI May 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi Evans Kidero ameshindwa katika jaribio lake la kutaka mahakama isikubali taarifa za benki zitumike kama ushahidi dhidi yake katika kesi ya sakata ya Sh58 milioni kutoka kwa serikali ya Kaunti ya Nairobi.

Wakati huo huo, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) iliambia mahakama kuwa Bw Kidero, katika taarifa yake ya ushahidi, alikiri kupokea Sh14.4 milioni kutoka kampuni ya Cups Limited, mojawapo ya kampuni zinazohusishwa na sakata hiyo.

Jaji Lucy Njuguna alikataa ombi la Kidero la kuzuia mpelelezi wa EACC, Bi Mulki Umar, kuwasilisha taarifa za benki kama ushahidi. Bi Umar ndiye aliyefanya uchunguzi wa akaunti hizo na kupata ushahidi unaomhusisha Kidero na washukiwa wengine 13, akiwemo Mbunge wa Nyakach Aduma Joshua Owuor, katika sakata ya fedha hizo mnamo Januari 2014.

Jaji aliamua kuwa hakuna sababu maalum ya kuhitaji afisa wa benki kuwasilisha taarifa hizo, hasa kwa kuwa Kidero mwenyewe alikiri kupokea kiasi hicho cha pesa.

“Pale ambapo vitabu vya benki vimepatikana kwa njia halali na mfumo wa uwasilishaji haujavunjika, hakuna upendeleo wowote wa mpelelezi kuwasilisha stakabadhi hizo. Isitoshe, Bw Kidero hajakanusha maelezo yoyote katika taarifa ya benki inayozungumziwa,” alisema Jaji Njuguna.

EACC iliwasilisha stakabadhi zikiwemo fomu za kufungua akaunti, taarifa za benki, kadi za mamlaka, vocha za kuweka pesa na vitabu vya benki.

Kidero alipinga akisema kuwa mpelelezi si mtayarishaji wa stakabadhi hizo za benki na hivyo hastahili kuziwasilisha. Wakili wake alisema kuwa kwa mujibu wa kibali, Bi Umar aliruhusiwa tu kuchunguza na kunakili stakabadhi hizo, na si kuzitumia kama ushahidi bila afisa wa benki kuhusika.

Hata hivyo, Jaji Njuguna alisisitiza kuwa mpelelezi anaweza kuwasilisha taarifa hizo chini ya Kifungu cha 177(2) cha sheria.

Kesi hiyo ilifunguliwa mwaka 2021, na washtakiwa wengine 13 ni pamoja na aliyekuwa Diwani Paul Mutunga Mutungi, aliyekuwa Mbunge wa Embakasi ya Kati John Ndirangu Kariuki, aliyekuwa Mkuu wa Wafanyakazi wa Kaunti George Wainaina Njogu, kampuni ya The Cups Limited, na John Ngari Wainaina.

Wengine ni pamoja na Mbunge wa Nyakach, wahasibu wa zamani wa serikali ya kaunti Hannah Muthoni, Philomena Kavinya, Ng’ang’a Mungai (Ng’ang’alito), Ekaya Alumasi (Ghonzour), James Mimi Mbugua, Elizabeth Wanjiru Nderitu, na Alice Njeri Mundia.

Kesi inaendelea kusikilizwa.