Pigo kwa SHIF, seneti yakataa kanuni mbili za kutekeleza mpango huo
UTEKELEZAJI wa mpango mpya wa afya wa Rais William Ruto umepata pigo baada ya kamati ya Seneti kukataa mapendekezo ya sheria mbili za kuufanikisha.
Kamati ya Sheria ya seneti inayoongozwa na Seneta wa Tharaka Nithi Mwenda Gataya, imependekeza kanuni hizo zifutiliwe mbali kwani umma haukushirikishwa, jambo ambalo ni kinyume na ibara ya 118 ya katiba.
Sheria hizi mbili ni muhimu katika utekelezaji wa Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF).
Kamati inalaumu Waziri wa Afya Susan Nakhumicha kwa kushindwa kutoa maelezo ya kuridhisha kuhusu mfumo uliotumiwa kufikia mchango wa asilimia 2.75 ya mapato kama ada za SHIF na usalama wa data.
Mapendekezo hayo yalitolewa saa chache kabla ya Waziri Nakhumicha kutangaza kuongeza muda wa kuanza kwa SHIF kutoka Julai 1, 2024 hadi Oktoba mwaka huu, kumaanisha kwamba Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) itaendelea kutumika.
Usajili wa SHIF umepangwa kuanza Jumatatu.
Huku Bi Nakhumicha akitangaza kuongezeka kwa muda huo, pendekezo la kamati ya seneti huenda likachelewesha kutekelezwa kwa SHIF.
“Wizara ya Afya ilipewa muda wa kutosha na fursa ya kuwasilisha ushahidi wa ushiriki wa kutosha wa umma lakini hili halikutolewa kwa kamati,” Seneta Gataya anasema katika ripoti ya kamati yake.
Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi alisema kuwa usajili wa Wakenya katika SHIF kabla ya kanuni hizo kupitishwa ni kinyume cha sheria na katiba.
“Waziri hapaswi kujaribu kuendelea na usajili kwa sababu utakataliwa vikali,” alisema Bw Osotsi.
Awali, SHIF ilipangwa kuanza Aprili mwaka huu kabla ya kusongezwa hadi Julai 1, 2024.
“Kwa maandalizi ya kuanzishwa kwa Bima ya Afya ya Jamii na manufaa yake, ninatangaza kwamba usajili utaanza tarehe 1 Julai 2024,” Waziri Nakhumicha alisema.
Sheria na Kanuni za SHIF zinalenga usajili mpya wa Wakenya na watu wote wanaoishi nchini Kenya.