Polisi 13 wafikishwa kortini kwa kuangamiza wataalamu wa uchaguzi afisi ya Ruto 2022
MAAFISA 13 wa polisi, afisa wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) na mlinzi wa Shirika la Huduma za Wanyamapori (KWS) Alhamisi, Februari 20, 2025 walishtakiwa katika Mahakama ya Kiambu kwa kuteka nyara na kuwaua raia wawili wa India na dereva wa teksi Mkenya mnamo Julai 22 na 23, 2022.
Maafisa hao 13 waliokuwa wa kitengo kilichovunjwa chini ya Idara ya Upelelezi wa Jinai, wanadaiwa kuwaua Nicodemus Mwania Mwange na raia wawili wa India waliotambuliwa kama Mohamed Zaid Sami na Zulfiqar Ahmed Khan.
Kumekuwa na madai kuwa Sami na mwenzake Ahmed Khan, walikuwa wamezuru Kenya kama sehemu ya kikosi cha kidijitali cha kampeni ya Rais William Ruto wakati huo akiwa naibu rais, kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.
Dereva wa teksi, Bw Mwange, ambaye aliuawa pamoja na wageni hao wawili, alikuwa akiwasaidia kwa uchukuzi, na serikali haijawahi kukataa maelezo kwamba wawili hao walikuwa katika kampeni ya uchaguzi wa Dkt Ruto.
Watatu hao waliuawa takriban mwezi mmoja kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.
Walioshtakiwa kwa mauaji hayo ni Peter Muthee Gachiko, Inspekta Mkuu wa Polisi; James Kibosek, Inspekta wa Polisi; Koplo Joseph Kamau Mbugua, David Chepchieng, Joseph Mwenda, John Mwangi, na Hillary Limo; na Konstebo Stephen Luseno, Simon Muhuga, Paul Njogu, Boniface Otieno, Elkana Njeru, na Fredrick Thuku.
Walishtakiwa pamoja na John Wanjiku Macharia (NIS) na Michael Kiplagat (KWS) na wakakanusha kuhusika na mauaji ya watatu hao.
Washtakiwa hao walifikishwa mbele ya Jaji Abigail Mshila, na timu ya waendesha mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) ikiongozwa na Everlyn Onunga, Augustine Gacharia, Victor Owiti, Allen Mulama, Benjamin Kelwon na Kennedy Amwayi.
Kesi itatajwa Machi 20 2025 kwa mwelekeo zaidi ikiwemo iwapo wanafaa kuachiliwa kwa dhamana.