Polisi wa Kware wahamishwa kaimu IG akiahidi kutatua fumbo la miili kwenye magunia
MAAFISA wote katika Kituo cha Polisi cha Kware, Embakasi, Nairobi, kilichoko karibu na timbo ambapo maiti nane zimeopolewa tangu Ijumaa, wamehamishwa huku uchunguzi kuhusu kisa hicho ukiendelea.
Kaimu Ispekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin jana walitangaza kuwa wapelelezi watahitaji angalau muda wa siku 21 kufichua kilichotokea katika eneo la tukio lililoko eneo bunge la Embakasi Kusini.
Bw Kanja alisema uhamisho wa polisi hao utatoa nafasi kwa maafisa wa upelelezi kuandaa ripoti ya haki na isiyopendelea.
“Nimewahamisha maafisa wote wa polisi waliokuwa wakihudumu katika Kituo cha Polisi cha Kware. Wakati kama huu mgumu tunasimama na jamii ya eneo hilo na tumejitolewa kufichua ukweli na kuwahakikisha kuwa wahusika wanaadhibiwa kwa mujibu wa sheria,” akasema kwenye kikao na wanahabari afisini mwake Jumba la Jogoo, Nairobi.
Bw Kanja pia alihakikishia umma kwamba uchunguzi kuhusu kisa hicho utafichua asili ya miili hiyo iliyokatakatwa na kuwekwa kwenye magunia kabla ya kutupwa ndani ya timbo hilo karibu na kituo hicho cha polisi.
Kufikia sasa, kaimu huyo wa Inspekta Jenerali wa Polisi alisema, mtu mshukiwa mmoja ametambuliwa na polisi wanamchunguza.
Bw Kanja alithibitisha kuwa maiti nane zimeopolewa kutoka kwa timbo hilo na kupuuzilia mbali madai ya wakazi wa eneo hilo kwamba zaidi ya maiti 20 zimepatikana.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa DCI Bw Amin alisema miili hiyo imeoza kwa kiwango tofauti, japo yote ilikatakatwa na kuwekwa ndani ya magunia.
“Aidha, miili hiyo yote ilitupwa sehemu moja katika timbo hilo ambamo takataka hutupwa,” Bw Amin akasema.
“Mbinu iliyotumika ni moja. Miaka yao ni kati ya 18 hadi 30. Wote ni wanawake. Na miili hiyo imepakiwa na kufungwa kwa njia sawa,” akaongeza.
Bw Amin alisema mauaji hayo ya kiajabu yamechangia kuibuliwa kwa nadharia nyingi kuhusu kile kilichochochea unyama huo.
Kwa mfano, alishangaa ikiwa wahusika ni wanachama wa kundi lenye itikadi fulani ambao hushiriki vitendo vya uhalifu au ikiwa ni wahalifu sugu wanaohusishwa na mauaji ya kikatili.
“Au kisa hiki kinahusiana na wahudumu wa afya waliopotoka na wanaojihusisha katika vitendo vya uhalifu?. Tunajaribu kufuatilia nadharia hizo zote katika uchunguzi wetu,” Bw Amin akasema.
Mkurugenzi huyo wa DCI alisema maafisa wa polisi wanakabiliwa na wakati mgumu kuendesha uchunguzi wao kwa sababu wananchi wanazua fujo kwa kujawa na hasira.
Kwa hivyo, Bw Amin alitoa wito kwa wakazi wa eneo la Kware kusitisha fujo na wawasaidie maafisa hao kutoka kitengo cha mauaji katika DCI kutekeleza majukumu yao.
“Wananchi washirikiane na maafisa wetu wanaoendesha uchunguzi kuhusu tukio hili. Asilimia 70 ya ufanisi wa uchunguzi wowote wa aina hutokana na ukaguzi wa kina wa eneo la tukio. Ikiwa wananchi wanavuruga hali katika eneo la tukio, huenda tusipige hatua katika uchunguzi wetu,” akaeleza.
Maafisa wa polisi pia wamehoji watu wa familia ya Josephine Owino, waliodai kujiwa na ndoto iliyowaelekeza kusaka mwili wa mpendwa wao katika timbo hilo.
Ilidaiwa kuwa kufikia Ijumaa Josephine alikuwa ametoweka kwa muda wa wiki mbili.