Polisi walijua mapema shughuli haramu zilizoendelea msituni Shakahola, asema shahidi
MAAFISA wa usalama walikuwa na nafasi ya kuepusha maafa ya watu zaidi ya 400 Shakahola iwapo wangefuatilia kwa undani ripoti za uvamizi wa eneo hilo mwaka wa 2021.
Imebainika mahakamani kuwa, salili za mapema zilizoonyesha kuwa shughuli haramu zilikuwa zikiendelea ndani ya Msitu wa Shakahola mapema mwaka wa 2021, zilipuuzwa na kupelekea watu zaidi ya 429 kupoteza maisha yao katika eneo hilo hilo miaka miwili baadaye.
Aliyekuwa afisa mkuu wa kituo cha polisi cha Lango Baya (OCS), Inspekta Hamara Hassan, alikiri mbele ya Mahakama ya Mombasa kwamba ripoti ya uvamizi, ugavi na uuzaji wa ardhi kiharamu iliripotiwa katika kituo chao mnamo Agosti 4, 2021, lakini kesi hiyo haikufuatiliwa zaidi kubaini waliohusika.
Bw Hassan alikuwa afisini siku hiyo wakati Bw Alfred Mwazeze kutoka Watamu na Bw Daniel Kitsao walipotembelea kituo hicho kuwasilisha malalamishi.
Wawili hao walijitambulisha kama wanachama wa kampuni inayosimamia shamba kubwa la Chakama Ranch.
“Bw Mwazeze, ambaye alikuwa katibu alilalamika kwamba ardhi ya kampuni hiyo ilikuwa inauzwa. Walitambua kipande cha ardhi ambacho walishuku kilikuwa kimeuzwa kilomita tatu kutoka Makutano ya Shakahola kuelekea Sala Gate a,” akasema Bw Hassan.
Kulingana na afisa huyo, aliwashauri wawili hao warekodi taarifa na Konstebo wa Polisi Ibrahim Ali ili suala hilo lifuatiliwe zaidi.
“Lakini waliniambia kuwa watanipigia simu baada ya kufanya kikao na kamati nzima. Waliondoka lakini hawakupiga simu kama walivyoahidi,” afisa huyo alisema wakati wa kuhojiwa na kiongozi wa mashtaka Mohamed Yassir.
Bw Hassan alisema aliwapigia simu watu hao lakini wakamweleza kwamba suala hilo sasa lilikuwa likishughulikiwa na Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Lango Baya (ACC).
Shahidi huyo alisema wawili hao walimwambia kuwa wamewahi kuwasilisha malalamishi hayo kwa chifu wa eneo hilo bila mafanikio.
Afisa huyo alisema hakufuatilia suala hili tena baada ya kufahamishwa kuwa ACC ya Lango Baya alikuwa ikiishughulikia.
“Hatukujua kilichokuwa kikiendelea msituni. Si kweli kwamba tulijua lakini hatukuweza kuthubutu kumkamata Paul Mackenzie,” akasema.
Huku akiongozwa na timu ya upande wa mashtaka inayojumuisha Jami Yamina, Alex Gituma, Victor Simbi, Victor Owiti, Betty Rubia, na Hillary Isiaho, afisa huyo alisema alifanya uchunguzi na kubaini kuwa ardhi inayomilikiwa na Mackenzie haikuwa yake.
“Ardhi inayojulikana kama Kwa Mackenzie ni mali ya Chakama Ranch. Mackenzie hana hatimiliki yoyote ya ardhi hii,” alisema.
OCS huyo wa zamani, hata hivyo, alibainisha kuwa hawakuweza kumshtaki Mackenzie kwa kosa lolote kwa sababu walioripoti hawakufichua majina ya wale walioukuwa wakiuza na kuuziwa ardhi yao.
Bw Hassan pia alikiri kwamba mshukiwa mkuu, Paul Mackenzie, aliripoti katika kituo hicho cha polisi mnamo Novemba 2022, chini ya OB NO 15/8/11/2022 saa kumi jioni, kuhusu mwanamke aliyedai kwenye mtandao wa kijamii kwamba alikuwa akisafirisha watu ndani ya msituni na kuwaua.
Hata hivyo, afisa huyo alisema hakuwa kazini siku hiyo, na kwa hivyo, suala hilo lilishughulikiwa na naibu wake.
“Ningependa kufafanua kuwa sikuwa katuoni wakati huo. Sikuwa kazini kuanzia Novemba 4 hadi 13, 2022. Niliporejea, sikujua kuliendaje hadi makaburi yaligunduliwa ilipogunduliwa Aprili 1, 2023,” aliambia Hakimu Mkuu Alex Ithuku.
Alifichua kwamba naibu wake, Inspekta Stanley Bet, ambaye alikuwa kazini wakati huo, alikabidhi ripoti ya Mackenzie kwa Konstebo wa Polisi Elizabeth Muchai.
“Baada ya kuuliza, nilibaini kuwa baada ya Mackenzie kuwasilisha taarifa hiyo, alielekezwa kwa askari mwingine ambapo alikutana na Konstebo wa Polisi Simiyu ambaye alimshauri andikishe taarifa kwa SCCIO Malindi ambako alihudumiwa na Sajenti Yator. Hakuna faili ya kesi iliyofunguliwa katika kituo cha polisi cha Lango Baya kuhusu suala hili,” akasema.
Bw Hassan, ambaye sasa anahudumu katika makao makuu ya polisi ya kaunti ndogo ya Kinango huko Kwale, alisema kuwa kituo cha polisi cha Lango Baya haikuwa na vifaa vya kutosha kushughulikia kesi ya Mackenzie kwa sababu ilihitaji utaalam wa mtandaoni ili kubaini chanzo cha chapisho hilo.
Shahidi huyo alikana kufahamu lolote kuhusu Mackenzie kabla ya kukamatwa kwake Aprili 2023, wakati makaburi ya halaiki yalipogunduliwa katika msitu huo ambapo walikuwa wamefahamishwa hapo awali kuwa watu wasiojulikana walikuwa wakigawa na kuuzia watu ardhi.
“Kwa mara ya kwanza nilimfahamu Mackenzie wakati ripoti ya mtoto aliyetelekezwa na wazazi ilipoandikishwa na nilikutana naye kwa mara ya kwanza tulipoenda kumkamata,” afisa huyo alisema.
Shahidi aliyetoa ushahidi wake siku ya Jumatatu na Jumanne, alifahamisha mahakama kuwa uongozi wa eneo hilo ulikuwa na taarifa kuhusu matukio katika msitu huo lakini haukufanya lolote kuzuia watu kufa kwa njaa.
Mackenzie na wenzake 93 wamekanusha mashtaka 238 ya kuua bila kukusudia, wakidai kuwa vifo vya Shakahola havihusiani na uhuru wa kuabudu na kukusanyika waliyokuwa wakiendesha msituni.
Wameshikilia kwamba mafundisho na imani yao yanatokana na Biblia.