Polisi wawili Wakenya wajeruhiwa Haiti wakidumisha amani
POLISI wawili kutoka Kenya wamejeruhiwa vibaya na genge hatari kule Haiti kwa muda wa wiki moja iliyopita.
Maafisa watatu waliambia Reuters kuwa majeraha hayo yanaongeza orodha ya wale ambao wamejeruhiwa huku genge likizidisha ushambalizi dhidi ya vikosi vya kudumisha amani Haiti.
Kenya ilituma polisi 1000 ambao ni sehemu ya vikosi vya usalama kutoka mataifa mbalimbali maarufu kama MSS vinavyopambana na magenge ili kurejesha udhabiti katika utawala wa Haiti.
Polisi Mkenya alifariki mnamo Februari 2025, huku MSS ikisema mwingine alikuwa ametoweka.
Maafisa watatu ambao waliomba wasitajwe kwa kuhofia kuadhibiwa, walisema inaaminika afisa huyo amefariki.
Katika makao makuu ya Port-au-Prince, maafisa hao walisema polisi wawili waliojeruhiwa, walipatikana na madhila hayo wakipiga doria.
Makao hayo makuu yamekuwa yakidhibitiwa na magenge hatari ambayo yamesababisha mauti ya maelfu tangu 2021.
Msemaji wa MSS Jack Ombaka alithibitisha kuwa polisi hao wawili wamepelekwa Jamuhuri ya Dominica kwa matibabu spesheli.
“Katika vita vyovyote lazima kuwe na majeraha au vifo,” akasema Bw Ombaka.
Maafisa watatu waliozungumza na Reuters walisema magenge hayo yalikuwa yamezidisha uvamizi dhidi yao na wakalalamika kuwa hawana zana za kutosha za kivita.
Walisema afisa mmoja alipigwa risasi kichwani baada ya risasi kupenya kofia ya usalama aliyovaa.
Mwingine naye alijeruhiwa kwenye sikio baada ya rasisi kupenya kioo cha gari la kivita walilokuwa ndani.
Ujumbe wa MSS unapanga kuelekea Washington wiki hii kulalamikia ubora wa vifaa vya ulinzi walivyopokezwa na Amerika.
Habari kuhusu safari hiyo ilitolewa na maafisa wa ngazi ya juu wa MSS kwenye mahojiano na Reuters.
Amerika imetoa ufadhili mkubwa na vifaa vya kivita kwa vikosi vinavyopambana na magenge Haiti.
Hata hivyo, Kenya imechangia robo tatu ya maafisa wanaodumisha usalama, mataifa mengine bado yakiwa hayajawasilisha maafisa wao.
“MSS inaendelea kupokea vifaa kutoka kwa mataifa mbalimbali na washikadau na kuna hakikisho kuwa vinafikisha viwango vinavyohitajika,” akasema Bw Ombaka.
Kenya imekashifiwa kwa kupeleka maafisa wake Haiti ili kujivunia sifa za hadhi kimataifa, lakini serikali imekuwa ikisisitiza kuwa msukumo wao ni janga la kibinadamu.