Habari za Kitaifa

Pombe ya mauti Kirinyaga: Jumla watu 10 wafariki

February 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA MWANGI MUIRURI

KAMISHNA mshirikishi wa eneo la Kati Fred Shisia ametangaza kwamba pombe ya sumu iliyobugiwa katika Kaunti ya Kirinyaga usiku wa kuamkia Jumanne imesababisha vifo vya watu 10 kufikia sasa huku idadi ya waliolazwa hospitalini ikipanda na kufika saba.

Kati ya hao saba hao waliolazwa, watano wamepofuka, akaongeza.

Bw Shisia aliyetembelea eneo hilo la Kangai aliagiza mkasa huo kufuatiliwa kwa kina kubaini kama kuna wengine ambao huenda wameaga dunia wakiwa majumbani mwao au katika hospitali.

Bw Shisia alitoa amri misako ifanywe dhidi ya pombe za mauti.

Hayo yanajiri huku duru za kuaminika zikidokeza kuwa mkasa huo umemchemsha nyongo Naibu Rais Rigathi Gachagua si haba.

“Bw Gachagua alipiga simu katika makao makuu ya usalama eneo la Kati na akaonyesha kutoridhishwa kwake kwa dakika 28. Alitoa kila aina ya onyo kwa maafisa ambao alisema wametepetea kazini,” mdokezi wetu akasema.

Bw Gachagua anaongoza harakati za vita dhidi ya pombe za mauti na pia ulevi kiholela.

Juhudi za Naibu Rais zinapata upinzani mkali kutoka kwa wamiliki wa baa na walevi.

Maafisa wa usalama wamekuwa wakilaumu serikali za kaunti kwa kutoa leseni za baa kiholela.

Aidha mahakama nayo inalaumiwa kwa kutoa hukumu nyepesi kwa washtakiwa wa kuvumisha ulevi na mihadarati.

Wenyeji wa Kamandi tayari wamechoma baa ya California ambapo inadaiwa hapo ndipo walevi walifanya kikao wakaitisha chupa moja, mbili za pombe iliyosababisha vifo vya watu 10 huku saba wakilazwa.

[email protected]