Raha juu ya raha: Kindiki kupokezwa rasmi unaibu kiongozi wa UDA
ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua leo atavuliwa rasmi wadhifa wa naibu kiongozi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) katika mkutano maalum wa Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) jijini Nairobi.
Kulingana na Mwenyekiti wa Kitaifa cha chama hicho tawala Cecily Mbarire wadhifa huo utatwikwa Naibu Rais Kithure Kithure aliyeingia afisini Ijumaa wiki iliyopita.
“Katiba yetu ya UDA inasema kuwa wadhifa wa naibu kiongozi unashikiliwa na Naibu Rais. Kwa kuwa Rigathi Gachagua ametimuliwa na nafasi yake kutwaliwa na Profesa Kithure Kindiki hafai kuendelea kushikilia cheo hicho,” akasema.
“Kwa hivyo, Jumatatu tutakutana kama NEC na kumkabidhi rasmi Profesa Kindiki kiti cha naibu kiongozi wa chama chetu,” Bi Mbarire akasema Ijumaa katika uwanja wa KICC wakati wa sherehe ya uapisho wa Profesa Kindiki.
Mwenyekiti huyo wa UDA, ambaye ni Gavana wa Embu, alisema hayo siku chache baada ya Katibu Mkuu Hassan Omar kusema kuwa chama hicho hakitakubali Bw Gachagua kuendelea kushikilia wadhifa wa naibu kiongozi wa UDA.
“Tutamtawaza Naibu Rais Mteule Kithure Kindiki kuwa naibu kiongozi wa chama baada agizo la kusimamisha kuapishwa kwake kuondolewa. Hatuwezi kuruhusu Gachagua kuendelea kuwa nasi kwa sababu amekuwa akipinga sera za serikali,” Bw Omar akawaambia wanahabari katika makao makuu ya UDA, Nairobi.
Mnamo Alhamisi jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu walioondoa agizo lililotolewa na Jaji Richard Mwongo wa mahakama ya Kerugoya kuzuia kuapishwa kwa Profesa Kindiki.
Uamuzi huo wa majaji Eric Ogolla, Anthony Mrima na Freda Mugambi ulitoa nafasi ya kuapishwa rasmi kwa Profesa Kindiki kuanza kutekeleza majukumu ya Afisi ya Naibu Rais.