Habari za Kitaifa

Raia wana imani zaidi na viongozi wa kidini kuliko asasi za serikali- Utafiti

Na  LINET OWOKO January 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKENYA wanaendelea kukerwa na mkondo ambao nchi imechukua huku imani yao kwenye utendakazi wa asasi mbalimbali ikishuka maradufu.

Shirika la Utafiti Afrika linalofahamika kama Afrobarometer, limeonyesha kuwa Wakenya sasa wana imani ya juu kwa viongozi wa kidini na jeshi na hawaamini wanasiasa pamoja na asasi za serikali.Kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita, imani yao katika utendakazi wa umma imeshuka hadi asilimia 47.

Hali hii imechangiwa na ufisadi, kukosa kutimizwa kwa ahadi na pia ukosefu wa uwajibikaji.

“Imani ya watu imeshuka na ukitathmini asasi kama ya Rais, Bunge na Mahakama, imani ipo chini katika utendakazi wao,” ikasema ripoti hiyo.

Kumekuwa na imani kuwa asasi hizo tatu sasa zinadhibitiwa na utawala wa Rais William Ruto kiasi kuwa zimeibuka kibaraka cha utawala wake.Viongozi wa kidini wamegeuka kipenzi cha Wakenya huku imani kwao ikipanda hadi asilimia 72.

Jeshi halijaachwa nyuma na sasa linaaminika kwa asilimia 66.Kinaya ni kuwa mahakama, idara ya polisi, uongozi wa kisiasa na serikali za kaunti sasa haziaminiki sana na Wakenya.

Mahakama ambayo ilifahamika kama kimbilio kwa Wakenya sasa imeshuka, imani ikiwa ni asilimia 44 pekee ya wanaoamini kwenye utendakazi wake.

Kwenye tafiti za nyuma, mahakama ilikuwa na asilimia 47 lakini imani imeshuka kutokana na ufisadi ambao umekuwa ukishuhudiwa na kukithiri mno kwenye idara hiyo.

Polisi wanaaminika kwa asilimia 34 pekee huku ufisadi, matumizi ya nguvu kupita kiasi wakati wa maandamano na utendakazi duni ukichangia hilo.

Urais nao hauaminiki huku imani ya Wakenya ikiwa ni asilimia 52 kati ya 2011-2023. Asilimia hiyo imeshuka kwa alama nane.Imani kwa vyama vya kisiasa imeshuka hadi asilimia 32 huku serikali za kaunti na bunge zikiwa na asilimia 35 na 45 mtawalia, ambazo pia ni za chini kuliko za hapo awali.

Upinzani unaendelea kulemewa katika majukumu yao ya kuitia mizani serikali, Wakenya wakikosa kuamini utendakazi wao kwa asilimia 31.

Kukosekana huku kwa uaminifu kunaonyesha kuwa kuna shida katika taasisi za utawala Kenya. Hii imesababishwa na ufisadi, ukosefu wa uwajibikaji na kukosa kutimiza matakwa ya wananchi

“Ikiwa umma hauna imani katika utendakazi wa serikali basi ni vigumu kuwe na nia nzuri katika kutimiza malengo mbalimbali. Hii ndiyo maana Wakenya sasa wameweka imani yao kwenye jeshi na viongozi wa makanisa ambao hawahusiki moja kwa moja katika utekelezaji wa miradi,” ikaongeza ripoti hiyo.

Tangu mwaka jana, idadi ya visa vya utekaji nyara na ukosefu wa usalama vimeongezeka. Kumeibuka maswali kutoka kwa mashirika ya haki, makundi ya haki kuhusu utekaji nyara, serikali imekuwa ikidaiwa kuhusika.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, kumekuwa na ongezeko la asilimia 44 za utekaji nyara kati ya Septemba 2023 na Agosti 2024. Tume ya Kitaifa ya Kupambana na Haki za Kibinadamu iliripoti kuhusu zaidi ya visa 82 vya utekaji nyara ambavyo vilitokea mnamo 2024.

IMETAFSIRIWA NA CECIL ODONGO