Raila aambia Nyanza kwaheri akienda kujitosa kabisa siasa za bara Afrika
KIONGOZI wa upinzani Raila Odinga Jumapili alionekana kuaga ngome yake ya kisiasa ya Nyanza huku ili kumakinikia kampeni zake za uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) ambao uchaguzi wake ni Februari mwakani.
Bw Odinga alizindua rasmi kampeni zake za AUC mnamo Jumamosi ambapo aliweka maazimio yake kwa Bara la Afrika, akiahidi mageuzi makubwa akichukua wadhifa huo wa hadhi mno.
Jana, Bw Odinga aliwaambia wafuasi wake kuwa sasa safari yake ya AUC imeanza ila ameiacha chama chake cha ODM katika mkono salama huku akisema kuwa atakuwa tayari kutoa mwelekeo kwa uongozi mpya.
“Sitaenda milele. Nipo hapa nanyi bado. Ni dhahiri kuwa naenda AU lakini bado nitakuwa nanyi na nipo sana,” akasema Bw Odinga.
Alikuwa akiongea katika Shule ya Upili ya Ligisa, eneobunge Rangwe wakati wa hafla ya shukrani iliyoandaliwa na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga baada ya kuteuliwa kwake kama mwenyekiti wa kitaifa wa ODM.
Hapa nchini, Bw Odinga alizindua kampeni yake ya uenyekiti wa AUC mnamo Agosti 27. Uzinduzi huo uliandaliwa katika Ikulu ya Nairobi na kuongozwa na Rais William Ruto pamoja na marais wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (AUC).
Tangu uzinduzi huo, Bw Odinga amekuwa mara nyingi yuko nje ya nchi akizuru mataifa mbalimbali kusaka uungwaji mkono na pia kuhudhuria makongamano ambayo masuala ya Afrika yamekuwa yakijadiliwa.
Katika kinyángányiro cha AUC, Bw Odinga anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Djibouti Mahmoud Ali Youssef. Sheria za AU zinahitaji mwanizi wa cheo cha AUC ajiondoe kutoka kwa siasa za nyumbani na hilo lina maana kuwa Raila hatakuwa akijihusisha na siasa za ODM.
Eneo la Nyanza limekuwa ngome ya kisiasa ya Bw Odinga tangu 1994 baada ya kifo cha babake marehemu Jaramogi Oginga Odinga na waziri huyo mkuu alisema kuwa wanasiasa kutoka eneo hilo wanastahili kuungana hata akielekeza macho kwenye siasa za Afrika.
Akiwahutubia wafuasi wake kuhusu uchaguzi wa mashinani wa chama ambao utaandaliwa mwezi huu akiwa amemakinikia kampeni za AUC, waziri huyo mkuu wa zamani aliwataka watakaoshindwa nao wakubali na kuwauunga washindi.
Alisema ni kupitia makubaliano kama hayo ndipo chama kitaendelea kuwa imara na umoja hata akiwa AU huku akiwataka wafuasi wake wasiingiwe na hofu kuwa atakuwa akihusika na masuala ya Afrika pekee.
“Wanachama wote wa ODM wana maono moja na wote lazima washiriki uchaguzi huu. Kura hii itaanza mashinani kabla ya kuelekea hadi nafasi za juu ambapo wajumbe wataamua viongozi wa chama,” akasema Bw Odinga.
Bi Wanga alipokezwa wadhifa wa uenyekiti wa ODM baada ya John Mbadi kuteuliwa kama Waziri wa Fedha. Bw Mbadi na waliokuwa viongozi wa ODM Hassana Joho, Wycliffe Oparanya na Opiyo Wandayi waliteuliwa kwenye utawala wa Rais William Ruto baada ya maandamano ya vijana nchini miezi mitatu iliyopita.
Viongozi wa ODM kutoka Nyanza wakiwemo Gavana wa Siaya James Orengo na Kiongozi wa Wachache kwenye Bunge la Kitaifa Junet Mohamed, walimpigia debe Bi Wanga, wakisema wana matumaini atahakikisha Nyanza inasalia nyuma ya chama hata Raila akiwa AUC.
“Chama pekee ambacho kitastahimili mawimbi makali ni ODM. Kwa hivyo, lazima tuilinde na hatutajiunga na vyama vingine ila vyama hivyo ndivyo vitajiunga nasi,” akasema Bw Orengo. Bw Mohamed naye alisema Bi Wanga hata anatosha kuwa kiongozi wa chama.
Jana, Raila aliombewa na viongozi wa kidini kutoka Nyanza waliompa baraka ili ashinde uenyekiti wa AUC huku wale wa kisiasa nao wakimhakikishia ODM itakuwa imara hata akiwa Addis Ababa.
“Kazi yetu sasa ni kuhakikisha kuwa chama kina wawakilishi kwenye nyadhifa mbalimbali. Baba (Raila) tutaendelea kujenga chama na kukiimarisha kiumaarufu,” akasema Bi Wanga.
Manaibu viongozi wa ODM Simba Arati na Abdulswamad Nassir walimwaahidi Raila kuwa hata anapoelekea AUC watahakikisha kuwa kuna nidhamu chamani.
“Hatutaruhusu mtu yeyote kuvuruga chama na ODM itakuwa na wawaniaji kwenye nyadhifa zote za uongozi mnamo 2027,” akasema Bw Arati.