Raila kwa Gachagua: Sitaki unafiki, sitamuacha Ruto
KIONGOZI wa Orange Democratic Movement (ODM), Raila Odinga amemsuta aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua akimtaja kama ‘mwanasiasa mwenye unafiki’.
Kwa muda, hasa baada ya kubanduliwa 2024 kama naibu wa rais, Bw Gachagua amekuwa akimchumbia Waziri Mkuu huyo wa zamani akimtaka ajiunge naye kuanzisha mrengo wa kisiasa.
Gachagua ameahidi kuunda chama cha kisiasa kufikia Mei mwaka huu, anachodai kitatumika kumenyana na Rais William Ruto – kwa lengo la kumuondoa usukani.
Gachagua amekuwa mpinzani mkuu wa Rais Ruto, baada ya kuondolewa madarakani mwaka jana.
Rai za mbunge huyo wa zamani Mathira, hata hivyo, Bw Raila amezikataa akidai Gachagua ni “mnafiki”.
“Kuna wengine wanasema tuende upande wao ati ni mzuri. Jana (akimaanisha zamani) wewe ulikuwa unasema sisi ni nyang’au. Leo unasema tumekuwa malaika… Tumebadilika aje kutoka nyang’au hadi malaika?” Bw Odinga akasema.
Bw Raila Odinga ambaye kwa sasa anashirikiana sako kwa bako na Dkt Ruto, amesema Gachagua ni kiongozi mnafiki huku akirejelea baadhi ya matamshi yake akiwa mamlakani akimlima kisiasa.
“Hatutaki wanafiki, unakumbuka ukiweka mitego kila mahali ati ninaswe?” Odinga akahoji.
Alitoa matamshi hayo Jumatano (Machi 19, 2025), aliposhiriki chakula cha jioni – Iftar na kundi la jamii ya dini ya Kiislamu, ambayo inaendelea kusali Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Akiskika kumcheka Gachagua baada ya kubanduliwa 2024 na Bunge la Kitaifa na baadaye kutiwa muhuri na lile la Seneti, Raila Odinga alisema mitego ambayo Gachagua alimuwekea imemnasa mwenyewe.
Akiwa madarakani, Gachagua alinukuliwa akisema yeye ni mlinzi wa Serikali ya Kwanza kiasi cha kuzuia Raila kuingia Ikulu.
“Waswahili husema mtego wa panya hunasa walikuwemo na wasiokuwemo…” Bw Raila alimsuta Gachagua.
Gachagua aliondolewa usukani kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na kudunisha bosi wake.
Ni hatua ambayo imeonekana kukera baadhi ya wandani wa Gachagua kutoka Mlima Kenya, na hata kupandisha joto la kisiasa ngome yake.
Bw Odinga amekuwa akihoji uhusiano wake na Rais Ruto ulilenga kumuokoa aboreshe taifa, kufuatia kero ya vijana wa Gen Z Juni 2024 ambapo walitishia kumbandua kupitia maandamano ya kupinga kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2024 na uongozi waliotaja kuwa mbaya.
Dkt Ruto, hata hivyo, alifutilia mbali mswada huo unaoonekana kurejeshwa kwa njia fiche kupitia machapisho kwenye Gazeti Rasmi ya Serikali.
Bw Odinga na Ruto wamefanya handisheki ambayo imepelekea baadhi ya wandani wa kiongozi huyo wa ODM kuteuliwa mawaziri.