Raila: Nilivyookoa Rais Ruto dhidi ya mapinduzi ya jeshi
KINARA wa Upinzani Raila Odinga amefichua kuwa aliamua kumwokoa Rais William Ruto wakati wa maandamano ya Gen Z ili kuzima mapinduzi ya kijeshi ambayo yalikuwa yamesukwa na yalikuwa yakikaribia tu kutekelezwa.
Bw Odinga amekuwa akikosolewa na vijana nchini kuwa aliteka nyara wimbi lao la mageuzi, akalisambaratisha kisha akaungana na utawala wa Kenya Kwanza uliokuwa ukiwanyanyasa.
Akihojiwa na Taifa Leo nyumbani kwake mtaa wa Karen mnamo Ijumaa, waziri huyo mkuu wa zamani alifunguka na kusema alipigiwa simu na ‘rafiki’ ambaye alimwomba aingilie kati kwa sababu jeshi lilikuwa likielekea kung’oa utawala wa Rais Ruto maandamano yangeendelea kuchacha.
Waziri huyo mkuu alisema kuwa baada ya Bunge la Kitaifa kuvamiwa mnamo Juni 25 na vijana kuanza maasi yao kwa kulenga Ikulu, ilikuwa dhahiri kwamba utawala wa Kenya Kwanza ulikuwa ukielekea kuporomoka.
Hali hiyo ililazimu Rais kuagiza majeshi yatoke kwenye makao yao ili yahakikishe kulikuwa na utulivu na amani nchini baada ya polisi kulemewa na vijana.
“Ruto anaweza kuondolewa tu kupitia uchaguzi mkuu lakini unajua wanajeshi wakitoka kwenye kambi yao huwa hawarejei,” akasema Bw Odinga wakati wa mahojiano hayo.
Kiongozi huyo alifananisha hali ambayo Kenya ilijipata na yaliyotokea Misri wakati ambapo kundi la Kiislamu la Muslim Brotherhood lilimwondoa mamlakani Rais Hosni Mubarak.
Akiwa waziri mkuu, Bw Odinga alikuwa amemtembelea Rais Mubarak mnamo 2011 kujadili masuala ya Mto Nile wiki moja kabla ya kubanduliwa kwake. Alisema kiongozi huyo alimweleza hali ilikuwa shwari licha ya kuwa maandamano yalikuwa yametanda lakini akashangaa alitimuliwa siku chache baadaye.
Licha ya Muslim Brotherhood kumwondoa Rais Mubarak mamlakani, walikubali jeshi lichukue uongozi ili Abdel Fattah el-Sisi ambaye alikuwa waziri wa ulinzi aongoze kwa muhula moja kisha arejeshe mamlaka kwa raia.
“Hadi sasa bado yupo mamlakani na alipoingia madarakani alibadilisha sheria na kusalia madarakani,” akasema Bw Odinga huku akisema hayo ndiyo yalielekea kutokea hapa Kenya jeshi lingechukua mamlaka.
Kiongozi huyo wa upinzani alisimulia jinsi alivyotumia ushawishi wake wa kisiasa kuhakikisha Rais anatupilia mbali Mswada wa Fedha 2024 ambao ulikuwa unapingwa na vijana nchini.
Hata hivyo, alishutumu Gen Z kwa kukataa kushiriki mazungumzo na Rais Ruto ili masuala ambayo walikuwa wakilalamikia yashughulikiwe.
“Nilipendekeza mazungumzo ya kitaifa ambayo yangeshirikisha vijana kati ya 3,000- 5000 kutoka maeneo yote nchini. Vijana hao wangekuwa kati ya umri wa miaka 18-35 na asilimia 45 wangepewa nafasi serikalini lakini wakakataa,” akasema kiongozi huyo wa ODM.
Baada ya vijana kukataa, aliwafikia vinara wenzake katika Muungano wa Azimio na kuwashauri waungane na Rais Ruto serikalini lakini nao pia wakakataa.
“Sikusaliti Gen Z au kuungana na Ruto bila ufahamu wa wenzangu. Wao ndio walikataa lakini nilichofanya kiliokoa serikali na taifa letu kwa jumla,” akasema.
Kuhusu ushirikiano wa sasa na serikali, Bw Odinga ameutaja kuwa bora zaidi na mkataba walioutia saini na Rais unalenga kukabili changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikizonga nchi.