Habari za Kitaifa

Raila, Wandayi wageuzwa vibonzo vya kejeli baada ya Rais kuzamisha Adani waliyoitetea

Na BENSON MATHEKA, CHARLES WASONGA November 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto amesalimu amri na kubatilisha dili tata za mabilioni ya pesa za kampuni ya Adani Group kutoka India baada ya mwenyekiti wake Gautam Adani kufunguliwa mashtaka ya ufisadi jijini New York, Amerika.

Serikali ilikuwa imeapa kuendelea na mkataba wa Sh96.68 bilioni wa kujenga miundomisingi ya kusambaza umeme na kampuni tanzu ya Adani, Adani Energy Solutions Limited licha ya Gautam Adani na maafisa wakuu wa kampuni yake kufunguliwa mashtaka Amerika.

Kushtakiwa kwake kunajiri baada ya serikali ya Kenya kutetea kandarasi ambazo imetoa kwa kampuni hiyo.

Rais William Ruto, kiongozi wa ODM Raila Odinga na mawaziri Davis Chirchir na Opiyo Wandayi walikuwa wametetea mikataba ya Kenya na kampuni hiyo licha ya kupingwa kortini kwa madai ya kukosa kushirikisha umma kikamilifu na habari kwamba, imelaumiwa kwa ukosefu wa uadilifu katika mataifa mengine.

Katika hotuba yake kwa Bunge Alhamisi, kiongozi wa nchi alisema Serikali haingeweza kuendelea na mikataba ya ushirikiano na Adani, baada ya kupata ushahidi wa ufisadi kuihusu.

“Nimewahi kusema huko nyuma, na narudia tena leo kwamba, nikipata ushahidi usio na shaka au taarifa za kuaminika kuhusu hongo, sitasita kuchukua hatua madhubuti.

“Kwa mantiki hiyo, sasa naelekeza – katika kuendeleza kanuni zilizoainishwa katika Ibara ya 10 ya Katiba kuhusu uwazi na uwajibikaji, na kwa kuzingatia taarifa mpya zilizotolewa na vyombo vyetu vya uchunguzi na mataifa washirika – kwamba idara za ununuzi ndani ya Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Kawi na Petroli zifute mara moja mchakato unaoendelea wa shughuli za upanuzi wa JKIA kupitia ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, pamoja na mkataba wa kujenga laini za usambazaji stima wa KETRACO uliokamilika hivi majuzi na kuanza mchakato wa kutafuta washirika mbadala,” Rais aliagiza.

Waendesha mashtaka Amerika

Waendesha mashtaka wa Amerika walisema Jumatano kwamba, Adani na washtakiwa wengine saba, ikiwa ni pamoja na mpwa wake Sagar Adani, walikubali kulipa hongo ya takriban dola 265 milioni (Sh35 bilioni) kwa maafisa wa serikali ya India ili kupata kandarasi za zaidi ya dola 2 bilioni ya kuendeleza mradi mkubwa zaidi wa umeme wa jua nchini India.

Waendesha mashtaka wa Amerika walisema Adani na afisa mkuu wa kampuni ya Adani Energy, walikusanya zaidi ya dola 3 bilioni za kuficha ufisadi wao kutoka kwa wakopeshaji na wawekezaji. Washtakiwa wengine watano walishtakiwa kwa kula njama ya kukiuka Sheria ya Ufisadi, sheria ya Amerika dhidi ya rushwa, na wanne walishtakiwa kwa kula njama kuzuia haki.

Bw Adani, bilionea raia wa India, ni mwenyekiti wa kampuni ya India ya Adani Group inayomiliki kampuni ya Adani Energy Solutions Limited ambayo imekuwa ikishirikiana na Ketraco, shirika la serikali, kujenga laini za kusambaza umeme.

Agizo la Rais lilijiri chini ya saa moja baada ya Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi akiwa mbele ya kamati ya Seneti kuhusu Kawi, kutetea kampuni hiyo.

‘Tutaendelea na Adani’

Bw Wandayi alisema kuwa serikali itaendelea na mpango wa Adani chini ya Pendekezo la Kibinafsi (PIP) kulingana na Sheria ya Ushirikiano wa Sekta ya Umma na ya Kibinafsi (PPP) ili kuimarisha usambazaji wa umeme nchini licha ya wasiwasi kutoka kwa umma na Maseneta.

“Tutaendelea na Adani kulingana na ukaguzi uliofanywa katika awamu mbili kuhusu Adani Energy Solutions,” akasema Wandayi.

Lakini hata hivyo, maseneta Ledama Ole Kina (Narok), Edwin Sifuna (Nairobi), Bonny Khalwale (Kakamega) na Danson Mungatana (Tana River) walimuuliza serikali ilivyoamini kuwa kampuni hiyo haikuwa na rekodi za uhalifu.

Adani imewasilisha zabuni ya kuboresha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa kima cha Sh230 bilioni ambayo, kama ingefaulu, ingesimamia uwanja huo kwa miaka 30.

Kuna kesi kadhaa kortini kupinga mpango wa Adani kukabidhiwa JKIA ambapo serikali imeshtakiwa.