Rais ajisahaulisha mahangaiko ya wiki, aonekana mtulivu akihudhuria ibada kanisani
RAIS William Ruto ameonekana kuyasahau mashaka yaliyokumba utawala wake wiki iliyomalizika, kwa kuhudhuria ibada ya Jumapili katika kanisa la PEFA katika Kaunti ya Narok.
Akiandamana na Gavana Patrick Ntutu na gavana wa zamani Samuel Tunai, Kiongozi wa Taifa alionekana mtulivu akitangamana na waumini wengine katika kanisa hilo lililoko Lolgorian.
Jumanne, Juni 25, 2024 itabakia siku ya giza zaidi katika utawala wake ambao ndio unakaribia kufikisha miaka miwili, wakati waandamanaji wengi wao wakiwa vijana wachanga walipovamia na kuharibu Majengo ya Bunge katika mzozo kuhusu Mswada wa Fedha 2024.
Kulikuwa na malumbano kwa wiki nyingi kuhusu mapendekezo ya ushuru katika mswada huo, lakini upande wa serikali ulishikilia kwamba ni sharti upitishwe ili miradi iweze kuendelea.
Baadaye Rais Ruto aliita kikao na wabunge wa Kenya Kwanza na kukubaliana kuondoa baadhi ya vipengele haswa vilivyohusu ushuru wa mkate, magari, huduma za kutuma pesa miongoni mwa vingine.
Lakini hatua hiyo haikutosha kutuliza vijana waliotaka mswada huo uondolewe kabisa.
Mnamo Jumanne, wengi waliduwaa wakati kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya nchi hii, raia walilemea maafisa wa polisi na kuvunja ua wa Bunge na kuingia ndani. Hii ilikuwa muda mfupi baada ya wabunge kupiga kura kupitisha mswada huo tatanishi. Baadhi ya sehemu za majengo zikachomwa huku uharibifu usiomithilika ukidhihirika.
Dkt Ruto baadaye Jumatano alitangaza kuondoa mswada huo kufuatia ghasia zilizoshtua nchi na ambazo ziliishia katika mauaji ya waandamanaji takriban 50.