Rais azindua mtambo wa kuchakata mchele Kisumu
RAIS William Ruto amewataka wakulima wa mpunga katika eneo la Magharibi mwa Kenya kutumia vizuri mashine ya kisasa ya kutoa maganda ya mchele katika kituo cha Mamlaka ya Ustawi wa Eneo la Ziwa (LBDA) kilichoko Kibos, Kisumu kuimarisha kilimo cha zao hilo.
Akizindua mashine hiyo Jumamosi akikamilisha ziara yake ya siku nne eneo la Luo Nyanza, Dkt Ruto alielezea matumaini kuwa mashine hiyo itapiga jeki sekta ya kilimo cha mpunga eneo hilo.
“Sasa ninawahimiza wakulima wetu kutumia kikamilifu mashine hii ili kufaidika sawa sawa kwani hawatasumbuka kupeleka mavuno yao kule Uganda ili yaondolewa maganda. Mashine hii itapiga jeki sekta ya kilimo cha mpunga eneo hilo na kuimarisha uzalishaji wa mchele nchini kwa ujumla,” Rais akasema.
Inakadiriwa kuwa jumla ya wakulima 6,000 watapeleka mavuno yao katika kituo hicho ili yatolewe maganda na kupakiwa kabla ya kuuzwa.
Kwa muda mrefu wakulima wamekuwa wakiuza mchele ghafi kwa mabroka kwa bei duni licha ya wao kubeba gharama kubwa katika kilimo cha mpunga.
Machine hiyo mpya ina uwezo wa kutayarisha tani nne za mchele ghafi kwa saa ikilinganishwa na mashine ya zamani iliyonunuliwa 1996 yenye uwezo wa kutayarisha tano 3.5 ya mchele kwa saa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa LBDA Wycliffe Ochiaga alielezea mtambo huo upya utapiga jeki maendeleo katika eneo hilo.
“Mashine hii iliyonunuliwa na serikali kuu kutoka India katika mwaka wa kifedha uliopita utaleta mwamko mpya katika maendeleo eneo zima la ziwa ambako kilimo cha mpunga ni uti wa mgongo wa uchumi,” akasema.
“Mheshimiwa Rais mashine hii itasaidia pakubwa kuongeza thamani kwa mchele. Kwa mfano, sasa tutaweza kutengeneza lishe ya kuku na samaki kutokana na maganda ya mchele ghafi,” Bw Ochiaga akaongeza.
Afisa huyo pia aliishukuru serikali ya kitaifa kwa kutoa Sh100 milioni za kusaidia katika ununuzi wa mchele ghafi katika eneo hilo.
“Ili kuwasaidia wakulima wetu zaidi, tumeanzisha mpango wa kuwasaidia katika nyanja ya utayarishaji mashamba na uvunaji kwa kutumia mitambo ya kisasa,” Ochiaga akaeleza.