Rambirambi zatanda kwa aliyekuwa nahodha wa Harambee Stars Austin Oduor, babake kipa Arnold Origi
RISALA za rambirambi zinaendelea kumiminika kutokana na kifo cha aliyekuwa nahodha wa Harambee Stars na klabu ya Gor Mahia, Austin “Makamu” Oduor aliyeaga dunia Jumatano usiku hospitalini mjini Kakamega.
Akithibitisha habari hizo za kifo, ndugu yake Mike Okoth anayeishi Ubelgiji alisema: “Nimepokea habari za kifo cha Austin kwa masikitiko makubwa. Ni habari za kushtua na kuhuzunisha mno kwa sababu hakuwa mgonjwa.”
“Kifo chake ni pigo kubwa kwa jamii nzima. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi,” aliongeza Okoth aliyekuwa nahodha wa Harambee Stars miaka ya 90 na mapema 2000.
Mwishoni mwa wiki, Oduor alikuwa miongoni mwa majagina waliozuru Kaunti ya Siaya kuzipa nguvu timu za Dero FC na Siger FC katika uwanja wa Nyilima.
Hafla hiyo ilidhaminiwa na Eliud Owalo, Afisa katika Ikulu anayesimamia kitengo cha utendaji.
Oduor ni babake aliyekuwa kipa wa Harambee Stars Arnold Origi na mjombake mshambuliaji matata wa timu ya Ubelgiji, Divock Origi.
Oduor aliyekuwa nahodha wa Harambee Stars kati ya 1988 na 1990 anakumbukwa kwa kuongoza Gor Mahia walipoweka historia ya kuwa timu ya kwanza kutoka Afrika Mashariki na Kati kutwaa Kombe la Washindi (Mandela Cup) mnamo 1987.
K’Ogalo ilibeba kombe hilo mbele ya mashabiki 60,000 waliomiminika uwanjani MISC Kasarani, Nairobi baada matokeo ya jumla ya 3-3 dhidi ya Esperence Sportive de Tunis ya Tunisia. Gor waliibuka washindi kutokana na bao la ugenini.
Aliyekuwa mshambuliaji wa Harambee Stars, Sammy ‘Kempes’ Owino aliyeishi naye mtaani Ziwani, Nairobi alisema: “Alikuwa mtu mwadilifu. Alitetea haki. Niliporejea nchini baada ya kukaa nje kwa muda mrefu, nilimpata bado anashikilia maadili hayo.”
Aliyekuwa mshambuliaji wa Gor Mahia na Harambee Stars, Mike ‘Kwasa Kwasa’ Otieno alimtaja marehemu kama mtu aliyejali maslahi ya wengine.
“Nilipojiunga na Gor Mahia, nilikuwa mdogo kikosini. Lakini Austin alikuwa sura ya baba na alihakikisha hakuna ambaye alikosa kukidhiwa haja zake miongoni mwasisi tuliokuwa wadogo. Alikuwa nahodha bora kwa wote niliocheza chini yao,” alisema Otieno kuhusu Oduor aliyekuwa mwenyekiti wa kundi la Gor Mahia Legends Welfare Group.