Riggy G aalikwa kufika mbele ya wabunge ajitetee dhidi ya kutimuliwa
NAIBU Rais Rigathi Gachagua amealikwa kufika mbele ya wabunge Jumanne ijayo Oktoba 8, 2024, kujitetea kuhusu mashtaka 11 dhidi yake yaliyoorodheshwa katika hoja ya kumtimua afisini.
Kwenye taarifa kwa wabunge Jumanne jioni, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alisema Bw Gachagua pia anaweza kutuma mawakili kumtetea au aandamane na mawakili hao.
“Mheshimiwa Naibu Rais Rigathi Gachagua anaalikwa kufika bunge Jumanne Oktoba 8, yeye mwenye au akiandamana na wakili wake, kujitetea dhidi ya madai kwenye hoja hii. Atatengewa muda wa kufanya hivyo kati ya saa kumi na moja jioni na saa moja usiku,” akasema.
Aidha, Bw Wetang’ula alitangaza kuwa vikao vya kushiriki maoni ya umma kuhusu hoja hiyo vitafanyika Ijumaa, Oktoba 4, 2024 katika kaunti zote 47.
“Katika vikao hivyo, wananchi wa matabaka mbalimbali watapa fursa ya kutoa maoni na mapendekezo yao kuhusu hoja hii, kulingana na hitaji la Katiba. Hii ni kwa sababu hoja hii imevutia hisia kubwa kitaifa,” Spika huyo akaeleza.
Bw Wetang’ula pia alisema kuwa usalama wa wabunge 291 ambao walitia saini kuunga mkono hoja hiyo utaimarishwa “endapo kutakuwa na haja ya kufanya hivyo.”
“Mimi kama mwenyekiti wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC) niwasilisha ombi kwa Inspekta Jenerali wa Polisi ili awape walinzi zaidi wabunge watakaoniaeleza kuwa wanahofia usalama wao,” akaeleza.
Bw Wetang’ula alisema hayo baada ya kiongozi wa wachache mwenzake Junet Mohamed kumtaka kuhakikisha kuwa wabunge waliotia saini hoja hiyo wamelindwa wakati kipindi cha kushughulikiwa kwake.
“Mheshimiwa Spika ningetaka kupata hakikisho kutoka kwako kwamba usalama wa wabunge 291 ambao wametia saini hoja hii, pamoja na mdhamini, utaimarishwa. Sababu ni kwamba yule wanataka aondolewe afisini ni mtu mwenye nguvu zaidi kifedha na kimamlaka,” akasema Bw Junet ambaye pia ni Mbunge wa Suna Mashariki.
Mbunge wa Dadaab Farah Maalim naye alitaka usalama wa Rais William Ruto pia uimarishwe.
“Hatufai kuwalinda wabunge 291 waliotia sahihi zao katika hoja hii pekee, Inspekta Jenerali wa Polisi vile vile sharti ahakikishe kuwa Rais amelindwa sawasawa. Tunajua aina ya Katiba tuliyo nayo…. Mtu yeyote anaweza kuamua kubadili mkondo wa historia na kuamua kumdhuru Rais,” akasema Mbunge huyo aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha Wiper.
Awali, hoja hiyo iliwasilishwa bungeni rasmi na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse, ambaye ndiye mdhamini wake.
Mbunge huyo aliyechaguliwa Bungeni kwa tiketi ya Chama cha Maendeleo Chap Chap (MCC) alisema kuwa anayo ushahidi wa kutosha kuhimili makosa 11 aliyomwelekezea Bw Gachagua.
Miongoni mwa makosa hayo ni ukiukaji wa Katiba, haswa kipengele cha 10, kwa kuendeleza ukabila na ubaguzi.