Rita alinyongwa kabla kukatwakatwa, mpasuaji wa serikali asema
NA MARY WAMBUI
BI Rita Waeni alinyongwa kisha akakatwakatwa kabla ya vipande vya mwili wake kutupwa, mpasuaji wa serikali Johansen Oduor amefichua.
Akizungumza jana baada ya kufanya upasuaji kwenye kichwa kilichopatikana Kaunti ya Kiambu na kinachoaminika kuwa cha marehemu (baada ya kutambulishwa hivyo na familia yake) Dkt Oduor alisema uchunguzi unaashiria kichwa cha marehemu kilikatwa kuanzia shingoni.
“Utosi ulikuwa na jeraha ambalo kwangu linaonekana kama lililosababishwa na kifaa butu na baada ya kuchunguza viungo vya shingoni, tuliona mifupa iliyovunjika ambayo ni muhimu sana katika kesi ya mauaji. Hivyo basi kutokana na hayo yote ninaweza kuhitimisha kwamba kilichosababisha mauaji ya msichana huyo mchanga ni kunyongwa ambapo baadaye alikatwa vipandevipande kisha mwili wake ukatupwa,” alisema Dkt Oduor.
Soma pia Maafisa wasaka kichwa cha Rita Waeni
Halafu Washukiwa wa mauaji ya Rita Waeni, raia wa Nigeria walinunua shoka mtandaoni – Polisi
Mtaalam huyo alifafanua kuwa japo familia ya Bi Rita ilitambulisha kichwa chake kutokana na maumbile yake ikiwemo paji la uso, nywele na mpangilio wa meno, chembechembe zake zingali zinahitajika kufanyiwa uchunguzi katika maabara ya serikali ili kubaini iwapo zinalingana na sehemu nyinginezo za mwili.
“Kichwa kimeoza na ni sharti tutumie mbinu za kisayansi kubaini iwapo kweli ni cha mhasiriwa. Kuna chembechembe ambazo zitafanyiwa uchunguzi wa DNA ili kujaribu kuzilinganisha na zilizotolewa kwenye mwili uliopatikana,” alifafanua Dkt Oduor akiwa City Mortuary, Nairobi.
Majeraha kwenye kichwa na mifupa iliyovunjika shingoni huenda yalisababishwa na kifaa butu.
Upasuaji huo ulifanyika City Mortuary baada ya upasuaji wa awali uliofanyiwa sehemu nyinginezo za mwili wake wiki iliyopita.
Wauaji wa Rita walitupa kichwa chake kando na sehemu nyingine za mwili wake uliokatwa vipande vipande katika kinachoominika kuwa jaribio la kuficha ushahidi.
Mnamo Jumatatu, jamaa wa marehemu walithibitisha kuwa kichwa kilichopatikana ni chake baada ya kukitazama City Mortuary na kuona vifaa vilivyopatikana nacho katika Kituo cha Polisi cha Kiambaa, Kaunti ya Kiambu.
Makachero wamewakamata raia wawili wa Nigeria, William Ovie Opia na Johnbull Asbor wanaotuhumiwa kutekeleza mauaji hayo.
Wawili hao walifikishwa mbele ya Mahakama ya Makadara Jumatatu ambapo polisi waliomba kuwazuilia kwa muda wa siku nane ili kukamilisha uchunguzi.
“Raia hao wa kigeni wamepatikana kuwepo nchini kinyume na sheria kwa sababu nambari ya pasipoti ya William Ovie Opia, A08322863 imemaliza muda wa kutumika naye Johnbull Asibor hana pasipoti na anadai tu aliipoteza mwaka mmoja uliopita,” ilisema hati kiapo iliyowasilishwa kortini na Afisa wa Uchunguzi, Benjamin Wangila.
Wawili hao watasalia kizuizini hadi Jumatano wiki ijayo wakati polisi wanatarajiwa kuwasilisha kesi dhidi yao.
Wapelelezi wanaochunguza mauaji wamechukua ushukani na kutoa mwongozo kuhusu tarehe ya upasuaji utakaofuata huku uchunguzi kuhusu tukio hilo ukiingia wiki ya pili.
Mwili wa Rita ulipatikana Jumapili Januari 14, 2024.