• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Ruto aanza kupigia debe Raila apate kiti cha AUC

Ruto aanza kupigia debe Raila apate kiti cha AUC

Na JUSTUS OCHIENG

JUHUDI za Rais William Ruto za kumvumisha kiongozi wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga kama chaguo bora kwa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) jana ziliendelea kufaulu baada ya Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo kukubali kumuunga mkono kiongozi huyo wa upinzani.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Rais Ruto, ambaye yuko ziarani nchini humo, kumnadi rasmi Bw Odinga katika eneo la Afrika Magharibi.

Mwezi jana, Rais Ruto alitangaza kuwa marais wote wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wameidhinisha mpinzani wake mkuu wa kisiasa kwa wadhifa huo wenye hadhi ya juu Afrika.

Hata hivyo, ni mataifa ya Uganda na Rwanda ambayo yamejitokeza wazi wazi na kuahidi kumuunga Bw Odinga.

Akiongea jana wakati wa ziara yake nchini Ghana, Rais Ruto alisema Kenya imedhamini mwaniaji wa kiti hicho cha AUC kwa sababu imekuwa mstari wa mbele kutetea ajenda za kuboresha hadhi bara Afrika.

“….. hii ni katika nyanja za kupigania uhuru, amani, usalama, maendeleo na juhudi za kupambana na madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

“Tunataraji kufanyakazi na nchi zote huku tukilenga kufikia Ajenda ya Afrika ya 2063,” Rais Ruto akasema.

Alimshukuru mwenyeji wake, Rais Addo kwa kuunga mkono azma ya Kenya ya AUC.

Kwenye kikao cha pamoja na wanahabari, Rais huyo wa Ghana pia aliangazia jinsi taifa lake litafaidi kwa kuunga mkono mgombeaji kutoka Kenya.

“Mimi pia nimeomba uungwaji mkono kutoka kwa Rais Ruto kwa Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Ghana Mhe Shirley Ayorkor Botchwey kwa wadhifa wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola katika uchaguzi ujao utakaofanyika wakati wa mkutano wa Marais wa Nchini Wanachama wa Jumuiya ya Madola jijini Samoa mwaka huu,” Akufo-Addo akasema.

Kuna uwezekano mkubwa kwamba Rais huyo wa Ghana hatakuwa afisini wakati ambapo uchaguzi wa AUC na Katibu Mkuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola.

Anahudumu muhula wake wa mwisho kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Desemba mwaka huu.

Marais wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) wachagua mwenyekiti mpya wa AUC Februari mwaka ujao. Kwa upande mwingine uchaguzi wa Jumuiya ya Madola utafanyika Septemba mwaka huu.

“Nakushuru zaidi Mheshimiwa Rais kwa kukubali kuunga mkono mgombeaji wa Kenya kwa kiti cha mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika kati ya 2025 hadi 2028. Hatua hiyo imeanzishwa kufuatia mashauriano ya kina miongoni mwa wadau katika mataifa mbalimbali,” Rais Ruto akaeleza.

Kiongozi wa taifa aliahidi kuwa Kenya itaunga azma ya Ghana kwenye kinyang’anyiro cha wadhifa wa Katibu Mkuu wa Mataifa Wanachama wa Jumuiya ya Madola kati ya 2024 hadi 2029.

Kufikia sasa imebainika kuwa Shiriley Ayorkor wa Ghana atashindana na mpinzani kutoka Lesotho.

“Hii inatoa nafasi ya ushirikiano kati ya Kenya na Ghana,” Dkt Ruto akasema.

Rais Ruto alikuwa anatarajiwa kuelekea Guinea-Bissau kwa ziara rasmi ya rais wa Kenya katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Vile vile, anatarajiwa kumpigia debe Bw Odinga akiwa huko.

  • Tags

You can share this post!

Aliyepandikiziwa figo ya nguruwe aruhusiwa kwenda nyumbani

Ahadi ya Ruto kugawia Taita-Taveta mapato ya mbuga ya Tsavo...

T L