Ruto aita Gen Z kwa mdahalo ili kushughulikia malalamishi yao
RAIS William Ruto amependekeza kuunda kikundi kushughulikia malalamishi ya vijana, kufuatia maandamano ambayo yalisababisha serikali kuitikia matakwa yao ya kuondoa Mswada wa Fedha 2024.
Kufuatia shinikizo kutoka kwa vijana, Rais William Ruto amependekeza kuundwa kwa Jukwaa la Kitaifa la Sekta Mbalimbali (NMSF) ili kushirikiana na washikadau wote katika kusuluhisha malalamishi hayo.
Jukwaa la Kitaifa la Sekta Mbalimbali (NMSF), rais alisema, litakuwa na wanachama kutoka kwa mashirika yote ya kitaifa yanayowakilisha vijana.
Kiongozi wa nchi aliomba mashirika ya kijamii, kidini, wataalamu, wafanyabiashara, wasomi, uongozi wa wanafunzi, viongozi wa walio wengi na walio wachache bungeni, Baraza la Magavana na makundi mengine ya wadau “kuteua wawakilishi watakaounda Kamati elekezi ya Kitaifa ya NMSF”.
Kulingana na taarifa kutoka kwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei, kila shirika la kitaifa linafaa kuteua wawakilishi wawili, mmoja kutoka kila jinsia ili kuzingatiwa kuteuliwa katika Kamati ya Kitaifa ya Uongozi.
Majina ya watakaoteuliwa, Bw Koskei alisema, yanapaswa kutumwa kwa Afisi ya Rais, Harambee House na yanapaswa kupokelewa kabla ya Julai 7, 2024 au siku hiyo.
Kamati ya uongozi ya kitaifa inayojumuisha watu 100, serikali ilisema, itakuwa chombo kikuu cha NMSF, chenye jukumu la kutoa mfumo, utaratibu, ajenda, na muda wa mazungumzo ya nchi nzima kuhusu masuala yaliyoibuliwa na vijana.
Mapendekezo hayo yanajiri huku vijana waliotamauka wakisisitiza kuwa hawana chama, hawana viongozi na hawana kabila.
Huku ikisubiriwa kuonekana yatakayojadiliwa, serikali ilisema, baadhi ya mambo ambayo yatashughulikiwa ni pamoja na ajira na fursa zingine, sera ya ushuru ya taifa, mzigo wa deni la taifa, uwakilishi na uwajibikaji, na kupambana na ufisadi miongoni mwa masuala mengine.
“Baada ya kuanzishwa kwa Kamati ya Kitaifa ya Uongozi ya NMSF, Rais atasimamia kikao cha kwanza cha kamati kutambua uongozi wa kongamano hilo,” Bw Koskei alisema. “Baadaye, kongamano hilo litafanya shughuli zake kwa uhuru katika kaunti zote 47 kupitia mchakato shirikishi, unaozingatia raia kuanzia wadi.”
Ingawa kamati itatoa mfumo na utaratibu wa kushirikiana na viongozi wa kisiasa kwa njia ya pande mbili, “kwa kuzingatia maadili ya kitaifa na kanuni za utawala wetu kuhusu ushirikishwaji wa umma, kila Mkenya na washikadau wote watapata fursa ya kuwasilisha mapendekezo yao kuhusu ajenda, maoni yao binafsi, au kama vikundi,” mkuu wa utumishi wa umma alisema.
Hata hivyo, kwa Rais Ruto, azma ya kuzungumza na vijana wasio na kiongozi, wenye hasira na wanaotaka kila mmoja asikike ni kibarua kinachomkosesha usingizi.