Ruto asemehe maelfu ya wafungwa wa makosa madogo na 56 waliotumikia vifungo virefu
RAIS William Ruto ametoa msamaha kwa Wakenya 56 na raia mmoja wa kigeni waliokuwa wakitumikia vifungo virefu gerezani, na hivyo kuwapa uhuru baada ya miaka mingi ya kifungo.
Rais pia alitoa msamaha wa jumla kwa wafungwa wote wa makosa madogo waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha hadi miezi sita, pamoja na wale wanaotumikia kifungo cha zaidi ya miezi sita lakini waliobakisha chini ya miezi sita kumaliza kifungo chao.
Tangazo hilo lilitolewa Jumatatu kupitia kwa Mkuu wa Wafanyakazi katika Ofisi ya Rais na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Bw Felix Koskei, katika taarifa rasmi.
Rais alitoa msamaha huo kwa kutumia mamlaka yake ya kikatiba ya huruma na msamaha chini ya Kifungu cha 133 cha Katiba ya Kenya, kufuatia mapendekezo ya Kamati ya Ushauri kuhusu Mamlaka ya Msamaha (PoMAC).
“Hatua hii ya rais inaakisi misingi ya marekebisho na haki ya kurejesha utu. Rais amewapa msamaha Wakenya 56 na raia mmoja wa kigeni waliokuwa wakitumikia vifungo virefu katika magereza mbalimbali nchini,” inasema taarifa hiyo ya Bw Koskei.
Masharti ya msamaha huo ni pamoja na kuachiliwa kwa masharti kwa wafungwa 31 waliokuwa wakitumikia kifungo cha maisha jela, pamoja na kuachiliwa na kurejeshwa nchi anayotoka raia mmoja wa nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) aliyekuwa akitumikia kifungo cha maisha.
Pia ni pamoja na kupunguziwa kifungo na kuachiliwa kwa watu 25, “ambao wataruhusiwa kuondoka gerezani baada ya kusamehewa sehemu ya kifungo chao kilichosalia.”
“Ili kuimarisha haki, Rais amewahimiza wadau wote wa mfumo wa haki ya jinai kutafuta mbinu bora zaidi za kutekeleza misingi ya maridhiano, marekebisho, urejeshaji na ujumuishaji katika jamii wahalifu waliomaliza kifungo,” taarifa hiyo ilieleza.