Habari za Kitaifa

Ruto asukumwa kumlinda Gachagua asidhulumiwe kisiasa

Na MWANGI MUIRURI September 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WANDANI wa Naibu Rais Rigathi Gachagua wameandaa malalamishi sita wanayodai yanasababisha misukosuko ndani ya serikali huku wandani wa Rais William Ruto katika eneo la Mlima Kenya wakipanga namna ya kupunguza ushawishi wa Gachagua eneo hilo.

Lakini Naibu Rais anaonekana kujiimarisha zaidi aneo hilo baada ya kupata uungwaji kutoka kwa Seneta wa Murang’a Joe Nyutu na Mbunge wa Gatanga Edward Muriu.

Wawili hao wamekuwa wakosoaji wake wakuu katika eneo la Mlima Kenya.

Sasa wandani wa Gachagua wanataka afisi yake iheshimiwe, isipunguziwe bajeti na serikali ikomeshe kampeni za kuhujumu juhudi zake za kupalilia umoja katika eneo la Mlima Kenya.

Gavana wa Nyeri amekuwa akisisitiza kuwa “tulisimama na Dkt Ruto alipokuwa akiteswa na bosi wake Rais Uhuru Kenyatta. Tunaamini Rais Ruto hataiga mfano huo wa kudhulumu naibu wake na washirika wake.”

Utekelezaji wa mikataba ya kiuchumi ambayo muungano wa Kenya Kwanza ilizindua katika Mlima Kenya na maeneo mengine kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 ni suala jingine wandani wa Gachagua wanataka serikali ilishughulikie.

Miongoni mwa yale yaliyomo katika mikataba hiyo ni mageuzi katika sekta za kilimo haswa kilimo cha majani chai, kahawa na ufugaji ng’ombe wa maziwa.

Rais Ruto alimtwika Bw Gachagua wajibu wa kufanikisha mageuzi katika nyanja hizo, kulingana na Agizo Rasmi la Rais alilotoa Januari 2023.

Mbunge wa Naivasha Jayne Kihara amelalamika kuwa kukatwa kwa bajeti ya kufanikisha mageuzi katika sekta ya kahawa kutoka Sh200 milioni hadi Sh6 milioni inalenga kuhujumu sekta hiyo.

“Tunataka kujua ikiwa kuna njama ya kimasukudi ya kulemaza juhudi za Gachagua za kufanikisha mageuzi katika sekta ya kahawa ili kumkosanisha na raia. Haifai kwamba utendakazi wa Gachagua unatarajiwa kuleta matokeo ilhali mgao wa fedha unapunguzwa,” Bi Kihara akasema.

Wandani wa Naibu Rais pia wanashinikiza kuwa polisi haswa wale wa Kitengo cha Upelelezi wa Jinai (DCI) wasitumike kisiasa kupitia visa vya utekaji nyara.

Wanataka vyombo vya dola visitumike na watu fulani kutisha Bw Gachagua na maagizo ya mahakama yaheshimiwe.

Wabunge Benjamin Gathiru (Embakasi ya Kati) na James Gakuya (Embakasi Kaskazini) wamelalamika kuwa DCI imekaidi agizo la mahakama kwamba warejeshewe simu zao.

Simu zao zilitwaliwa na maafisa hao wa upelelezi walipokuwa wakiendesha uchunguzi kuhusu wadhamini wa msururu wa maandamano ya kupinga serikali kati ya Juni na Julai.

“DCI isirejeshe nchi katika enzi ambapo viongozi wa kisiasa walikuwa wakidhulumiwa bila sababu maalum. Sharti wazingatiwa utaalamu na wapambane na wazingatie sheria wanapopambana na uhalifu,” Bw Gachagua akasema Jumapili.

Hii ni baada ya wabunge hao wawili kulalamika hadharani kuwa wanadhulumiwa na maafisa wa DCI.