Ruto ataambia nini wabunge na lawama zimezidi?
RAIS William Ruto anapotarajiwa leo kutoa hotuba yake bungeni kuhusu hali ya Taifa utekelezaji wa mipango na miradi ya serikali yake inaonekana kuyumba hali inayowakosesha matumaini raia.
Utekelezaji wa Mpango wa Afya kwa Wote (UHC) kupitia Bima mpya ya Afya ya Kijamii (SHIF) unayumbishwa na kasoro zinazoizonga bima hii iliyoanza kufanya kazi Oktoba 1, mwaka huu.
Kutokana na hitalifu hizo, wagonjwa wengi haswa wale wanaougua magonjwa sugu wanalazimika kulipia matibabu yao kwa pesa taslimu licha ya kusajiliwa na Mamlaka ya Afya ya Kijamii (SHA) inayosimamia bima hiyo.
Mpango wa Ujenzi wa Nyumba za Gharama Nafuu (AHP), uliotarajiwa kubuni nafasi za ajira haujafikia lengo hilo kwa ripoti za taasisi mbalimbali za serikali zinaonyesha kuwa kero la ukosefu wa ajira linaongezeka kila uchao.
Hii ni kwa sababu, kulingana na wadadisi, kampuni nyingi zinawafuta kazi wafanyakazi kutokana na kupanda kwa gharama ya uendeshaji shughuli kufuatia mwenendo wa serikali kupanda ushuru na matozo mengine kila mara.
“Kero la utovu wa ajira lingali donda sugu miaka miwili baada ya Rais Ruto kuingia mamlakani kwa sababu kampuni zinafuta wafanyakazi badala ya kuajiri. Kampuni zingine zinatamatisha shughuli zao Kenya na kuhamia mataifa jirani kwa kulemewa na gharama ya juu ya uzalishaji,” anasema Dkt Samuel Nyandemo, mwenyekiti wa idara ya mafunzo ya uchumi katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
Kampuni ya kibinafsi ya ulinzi ya G4S ndiyo ya hivi punde kutangaza kuwa inawafuta jumla ya wafanyakazi 400, shughuli itakayoanza Novemba 4, 2024 na kukamilika Aprili, 2025.
Kulingana na utafiti ulioendeshwa na Benki Kuu ya Nchini (CBK) Septemba mwaka huu, kampuni za kibinafsi zilifuta idadi kubwa zaidi ya wafanyakazi kuliko wale ambao ziliwaajiri.
Wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022, Rais Ruto (wakati huo akiwa naibu rais) aliahidi kuwa serikali yake ingelenga kuboresha uchumi ili uweze kuzalisha nafasi milioni moja za ajira kila mwaka.
Ahadi hiyo sasa imegeuka hewa kwani kulingana na ripoti iliyotolewa na Baraza la Kitaifa la Kusimamia Haki (NCAJ) ukosefu wa ajira ni sababu kuu iliyochangia ongezeko la visa vya uhalifu katika mwaka wa kifedha wa 2023/2024, baada ya Rais Ruto kuingia uongozini.
“Visa vya uhalifu mbaya vilipungua kati ya miaka ya kifedha ya 2019/20 na 2020/21 lakini vikapanda hadi 104,769 katika mwaka wa kifedha wa 2023/24,” ikasema ripoti hiyo.
Sekt ya elimu inakumbwa na changamoto nyingi, mfano ukiwa ni mgomo unaoendelea wa wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma. Wanafunzi wamesalia vyuoni kwa karibu wiki nne.
Kando na mgomo wa wahadhiri, vyuo vikuu vimekanganyikiwa baada ya serikali kusimamisha kwa muda utoaji wa fedha za kufadhili masomo ya wanafunzi chini ya mfumo mpya ulioanza kutekelezwa 2023.
Hii ni kufuatia agizo la Mahakama lililoamua kuwa mfumo huo mpya unakiuka sheria. Hayo yalijiri kufuatia malalamishi kwamba utekelezaji wa mfumo huo ujaa dosari kwani wanafunzi kutoka familia masikini wakiwekwa katika kundi la wanafunzi ambao wazazi wao wanajiweza.
Kulingana na Javas Bigambo, Rais Ruto leo anafaa kuwapa Wakenya matumaini serikali yake itarekebisha changamoto zinazowazonga Wakenya.
“Dkt Ruto atumie nafasi atakayopata Alhamisi bungeni kuelezea kwa kina mikakati ambayo serikali yake imeweka kukabiliana na changomoto hizo. Miaka miwili ni muda mrefu kwa Wakenya kusubiri, sasa awape matumaini kwamba Bima ya SHIF itafanyakazi, uchumi utaimarika na vijana kuanza kupata ajira humu nchini sio ng’ambo. Pia anapaswa kutoa hakikisho kuwa visa vya ukiukaji wa haki za kibinadamu kama vila utekaji nyara wa raia na sasa wageni utakoma,” anaeleza mchanganuzi huyo wa masuala ya siasa na uongozi.