Habari za Kitaifa

Ruto ataka mahakama ijizuie kutoa maamuzi yanayokwamisha utendakazi wa serikali

Na CECIL ODONGO November 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto, Jumatatu aliirai Idara ya Mahakama ijidhibiti ili isiwe ikitoa maamuzi ambayo yanaingilia masuala ya kitaifa na kutatiza utendakazi kwa umma.

Alisema baadhi ya maamuzi ambayo yamekuwa yakitoleawa huwa yanahujumu utendakazi wa serikali na kuwakosesha Wakenya huduma muhimu ya maendeleo.

“Utaweza kujibu vipi kesi ambapo watu wanapinga uwepo wa sera au wadhifa ambao umepigiwa kura na Wakenya?” akauliza Rais.

Alisema mahakama ina kibarua kikubwa cha kuhakikisha kuwa inasaidia nchi kuzima siasa za ubaguzi na kikabila na badala yake siasa ambazo zinahusu uwajibikaji kwa Wakenya ndizo zienezwe.

Matamshi haya yalionekana kumlenga aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ambaye aliondolewa mamlakani kutokana na hoja iliyowasilishwa katika bunge la kitaifa na seneti. Kati ya madai yaliyowasilishwa dhidi ya Bw Gachagua yalikuwa kueneza siasa za kikabila na kutenganisha nchi.

“Hakuna asasi au taasisi yoyote ya serikali ambayo inaweza kusimama kivyake bila kutegemea nyingine. Nini hufanyika wakati ambapo mahakama inaonekana kuingilia utendakazi wa asasi nyingine? Nani ataleta suluhu?” akauliza.

Rais Ruto alikuwa akiongea Jumatatu wakati wa kufungua Kongamano la Kuadhimisha miaka 12 ya uwepo wa Mahakama ya Juu jijini Nairobi.

Aliandamana na Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki, Kinara wa Mawaziri Musalia MudavadI, Jaji Mkuu Martha Koome, Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja miongoni mwa maafisa wengine wa ngazi ya juu serikalini.

Kiongozi wa nchi alitetea kanuni zinazotenga mamlaka katika asasi mbalimbali akisema lazima ziheshimiwe ili kuzuia mgongano wa majukumu. Alikiri kuwa kuna mwanya wa afisi ya Rais kuingilia ila hilo halimaanishi ihangaishwe mahakamani kupitia kesi ambazo huenda hazina mashiko.

Wakati wa hafla hiyo, Rais alisema kuwa ameshauriana na Bunge pamoja na Idara ya mahakama kuhusiana na bajeti na utawala wake utaunga mkono kupanuliwa kwa miundomsingi za mahakama kurahisisha upatikanaji wa haki.

Alitoa mfano wa matokeo tata ya uchaguzi mkuu wa 2007 ambapo alisema Mahakama ya Juu imesaidia kwenye utatuzi wa baadhi ya masuala tata yaliyoibuliwa kwenye kura hiyo na kusababisha machafuko.

“Miaka 12 baada ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Juu, si rahisi kufikiria jinsi taifa lilivyokuwa miaka mingi bila asasi hii muhimu,” akasema Rais.

Bi Koome aliwataka wanasiasa wavumiliane na waelewane kisha waje kortini kama hatua ya mwisho maridhiano yakikosekana. Alikariri kuwa suluhu za kisiasa ndiyo majibu ya kesi za kisiasa zinazowasilishwwaw kortini

“Mahakama ya Juu itaendelea kuwa na msingi imara ambayo itatetea na kulinda katiba ya nchi,” akasema Rais.