Habari za Kitaifa

Ruto avuna mfumo mpya wa ufadhili wa masomo ukihalalishwa na mahakama

Na SAM KIPLAGAT March 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NI afueni kwa serikali baada ya Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali uamuzi wa mahakama kuu uliozima mfumo mpya wa ufadhili wa masomo katika vyuo vikuu.

Hii ina maana kuwa serikali sasa iko huru kurejelea mpango wa utoaji wa mikopo na ufadhili chini ya mfumo huo ulioanzisha 2023.

Mawakili waliofika mbele ya majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa Jumatano, Machi 26, 2025 waliafikiana kuhusu aumuzi huo uliositisha utekelezaji wa uamuzi wa Jaji wa Mahakama Kuu Chacha Mwita.

Akitoa uamuzi wake mnamo Desemba 20, 2024, Jaji Mwita alisema kuwa mfumo huo mpya hautambuliwi kisheria na maoni ya kwa umma hayakushirikishwa kabla ya serikali kuanza kuutekeleza.

“Huku kusikizwa na kutolewa kwa uamuzi kuhusu rufaa kukisubiriwa, utekelezaji wa maagizo ya Mahakama Kuu yaliyotolewa Desemba 20, 2024 utasimamishwa,” majaji Patrick Kiage, Weldon Korir na Profesa Joel Ngugi wakasema.

Vile vile, pande husika zilikubaliana kwamba Mwanasheria Mkuu, Bodi ya Kutoa Mikopo kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (HELB), Wadhamini wa Hazina ya Vyuo Vikuu, zinawatangazia wanafunzi wote na wadau, njia za kukata rufaa zitakazotumiwa na wanafunzi wasioridhishwa na maamuzi kuhusu ufadhili au kuwekwa kwao katika makundi.

Pia soma https://taifaleo.nation.co.ke/habari/wanafunzi-uon-wavamia-afisi-za-helb-wakidai-pesa-tuk-nayo-yafungwa/

Majaji hao wa Mahakama ya Rufaa walisema kuwa hatua hiyo ichukuliwe ndani ya siku 14 kuanzia Jumatano, Machi 26.

Jaji Mwita alikuwa ametaja katika uamuzi wake kwamba asasi ambayo ilipaswa kupokea rufaa za wanafunzi haikujulikana, wanachama wake hawakujulikana na taratibu za utendakazi wake pia hazikujulikana.

“Inaweza kuwa asasi ya muda inayoweza kusikiza rufaa bila mpangilio wowote na kwa kuzingatia matakwa ya watu fulani,” Jaji Mwita akasema.

Jumatano, pande husika pia zilikubaliana kwamba wanafunzi na wadau wanapaswa kujulishwa kwamba mfumo huo wa ufadhili unaweza kubadilika siku zijazo, kutegemea matokeo ya rufaa hiyo.

Mahakama ya Rufaa iliagiza kwamba kesi hiyo iorodheshwe kusikizwa baada ya majaji kurejea kutoka likizo mnamo Aprili mwaka huu, 2025.

Tume ya Haki za Kibinadamu, Boaz Waruku, Elimu Bora Working Group na Muungano wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu ziliwasilishwa kesi kupinga mfumo huo mpya wa ufadhili wa masomo katika vyuo vikuu zikisema mfumo huo unahamisha wajibu wa kufadhili elimu kutoka kwa serikali hadi kwa wazazi ambao wanakabiliwa na hali ngumu kiuchumi.

“Ni wazi kwamba utekelezaji wa mapendekezo ya mfumo mpya wa ufadhili ulifanywa bila ushirikishwaji wa umma licha ya kwamba ulileta mageuzi makubwa katika ufadhili wa elimu ya juu nchini,” Jaji Mwita akasema.