Habari za KitaifaMakala

Ruto, Gachagua warejea mashinani kubembeleza mahasla

Na MWANGI MUIRURI August 18th, 2024 3 min read

RAIS William Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua sasa wamebadili mbinu za kushinda imani ya raia kwa kuanza kujitokeza katika nyumba za mahasla kula nao.

Katika muda wa wiki mbili zilizopita, rais na naibu wake wamechapisha picha zinazowaonyesha wakila chakula katika nyumba zisizo za kudumu za Wakenya wa tabaka la chini, wengi wao wakiwa wanawake.

Mnamo Agosti 9, 2024 wakiwa katika ziara ya kikazi katika Kaunti ya Murang’a, waliingia katika nyumba ya Bi Miriam Njeri eneo bunge la Mathioya ambapo baada ya kuwafungia nje wapiga picha isipokuwa wale wa idara zao za mawasiliano, walitoa picha zinazowaonyesha wakila mkate kwa chai.

Bi Njeri pia alinaswa katika video akiwaombea viongozi hao wawili wa kitaifa baada ya Rais Ruto kunadi sera ya umeme nchini mwaka wa 2024.

Sauti yake inasikika ikiitisha Sh300, 000 “kumpa mwanamke huyu na kumshukuru kwa ukarimu wake.”

Picha zao wakishiriki chai na mkate zimepamba kurasa rasmi za mitandao ya kijamii za viongozi hao wawili, haswa katika ziara zao za hivi majuzi za Mlima Kenya na eneo la Gusii.

Si jambo geni

Lakini kwa wawili hao, hili si jambo geni. Rais Ruto na Bw Gachagua walikuwa wakitangamana na watu wa kawaida wakifanya kampeni mwaka wa 2022.

Bw Gachagua pia amekumbatia mbinu hii. Akiwa nyumbani kwake Mathira, amekuwa akionekana akiongea na wananchi kando ya barabara, kushiriki chakula na vinywaji katika vyumba vya kupikia vilivyojaa moshi au kufanya matembezi ya asubuhi na wakazi.

Kurudia mbinu hizi kunaonekana kuwa jibu kwa shinikizo za vijana walioandamana kulalamikia utajiri ulioonyeshwa na baadhi ya wanasiasa na viongozi wa umma raia wengi wakikabiliwa na hali ngumu ya maisha.

Zaidi ya hayo, waandamanaji hao pia walipinga matumizi ya kanisa kufanya siasa.

Kulingana na Bi Margaret Njambi, 67, kutoka Kaunti ya Murang’a, kukutana kwake na viongozi hao kunabadilisha maisha.

“Nilikutana na Ruto mwaka wa 2021 na maisha yangu yakabadilika. Wakati wa kukutana naye, mapato yangu ya kila siku yalikuwa takriban Sh200. Alinipa pesa taslimu Sh500,000 na kunijengea nyumba ya kudumu ya Sh1 milioni,” aliambia Taifa Leo. Bi Njambi, hata hivyo, aliongeza kuwa hakupokea ng’ombe wawili wa gredi kama alivyoahidiwa.

“Mara tu wanasiasa hawa wanapokutana nawe, wanakuajiri kuwa balozi wao wa nia njema kwa kuwataja kama marafiki wa mtu wa kawaida,” alisema.

Bi Elizabeth Mugure anasema alikutana na rais wakati wa ziara ya Agosti 10, 2024 katika Kaunti ya Kirinyaga na ‘vivyo hivyo aliongea na msaidizi na bahasha ikatua kwangu.’

Alisema pengine rais aliguswa na mtoto aliyembeba wakati wa mvua ili kumshangilia alipozuru kaunti yao.

“Bahasha hiyo ilikuwa na Sh100,000. Kiasi cha juu zaidi ambacho nimewahi kuhesabu katika kikao kimoja ni Sh6,000 ambazo nilikuwa nimeweka akiba kwa miezi 18. Leo, hata kama Ruto anataka kutawala nchi hii maisha yake yote, nitampa kura yangu,” akasema.

Alifichua kwamba kabla ya ziara ya rais, uhamasishaji wa kichinichini ulikuwa umetangulia ‘ambapo kambi tatu zilikuwa zikitushawishi kushangilia kwa sauti zetu wakati wowote walipokabidhiwa kipaza sauti kuhutubu’.

Michael Mwiti 26, anasema alikuwa miongoni mwa vijana ambao katika soko la Kahuro eneo bunge la Kiharu walikuwa wamehamasishwa kukabidhi rais mbuzi.

“Tulikuwa tumepewa 60,000 kumnunua mnyama huyo, tulinunua kwa Sh24,000. Tuligawana zilizobaki. Yeye (Dkt Ruto) aliboresha maisha yangu na tukapamba mkutano wake,” akasema.

Hali ilikuwa sawa Jumatano wakati Rais na Naibu wake walipochapisha picha nyingine wakiwa wameketi katika chumba cha maakuli cha Bi Yunuke Nyanchongi 85, katika Kijiji cha Riasuta Itibonge katika Kaunti ya Kisii.

“Hapo awali, tuliwasha umeme nyumbani kwa Bi Nyanchongi, tulikula chakula nyumbani kwake na kwa shukrani akatuzawadi kuku,” yalisema maelezo ya picha.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Gasper Odhiambo anapuuzilia mbali mambo haya kama ‘kueneza utamaduni ambao ni upuuzi wa siasa zetu’.

Mbunge wa Githunguri, Bi Gathoni wa Muchomba, anasema vigogo hao wana tabia ya kutumia mahasla na kuwaacha katika hali ya kufadhaika.

Anatoa mfano wa Bi Pauline Waithera Njoroge aliyetumiwa katika kampeni ya hasla kisha akasahauliwa wawili hao walipoingia mamlakani kiasi cha kutoalikwa katika sherehe ya kuwaapisha kuingia ofisini.