Habari za Kitaifa

Ruto: Maandamano yaliyoshuhudiwa yalisheheni uhuni

Na SAMMY WAWERU November 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto ameonekana kutetea mienendo ya maafisa wa polisi waliodaiwa kuhangaisha waandamanaji Juni 2024, wakati wa maandamano dhidi ya serikali.

Kwenye hotuba yake kwa taifa Alhamisi, Novemba 21, 2024, Rais Ruto alisema licha ya serikali yake kuheshimu haki za Wakenya kuandamana, maandamano yaliyoshuhudiwa mwaka huu yalisheheni uhuni.

Juni 2024, vijana wa Gen Z walishiriki maandamano ya kitaifa kukosoa serikali – hasa baada ya kupitishwa kwa Mswada tata wa Fedha 2024.

Rais, hata hivyo, alifutilia mbali mswada huo uliopokea mapingamizi maeneo tofauti nchini.

“Tunaheshimu demokrasia na uhuru wa kujielezea, ila maandamano yaliyoshuhudia ilikuwa vigumu kutambua waandamanaji halali na wahalifu. Yalisheheni uhuni,” Dkt Ruto alisema, akihutubu bungeni.

Katika kauli iliyoskika anaunga mkono polisi kutumia nguvu kupita kiasi, kiongozi wa nchi alidai maafisa wa usalama walikabiliwa na wakati mgumu kulinda maisha ya watu, mali na biashara.

“Serikali itaendelea kulinda maisha ya watu na mali dhidi ya wahuni,” alisisitiza.

Hata ingawa Mswada wa Fedha 2024 Rais aliufutilia mbali, baadhi ya vipengele vinaanza kurejeshwa bungeni kupitia miswada.

Maandamano ya Juni, yalisababisha maafa ya vijana zaidi ya 60, mashirika ya kutetea haki za kibinadamu na wanaharakati wakinyooshea kidole cha lawama serikali ya Kenya Kwanza kwa kuendeleza utawala wa kiimla na utekaji nyara wa waandamanaji.

Baadhi ya waandamanaji waliotekwa nyara na maafisa wanaodaiwa kuwa wa polisi, hawajapatikana kufikia sasa.