Habari za Kitaifa

Ruto, mbunge wakemewa kuhusu zawadi ya Krismasi

Na CECIL ODONGO December 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

HATUA ya Rais William Ruto kuwapa wakazi wa Uasin Gishu vyakula vya Krismasi kwenye mifuko yenye majina na picha yake kuliibua maoni mseto katika mitandao ya kijamii.

Naye Mbunge wa Kisumu ya Kati Joshua Oron kuwapeleka mbuzi, kondoo na vyakula kama zawadi ya Krismasi nyumbani kwa Raila Odinga pia kuliibua hisia mseto, wengi wakihoji iwapo kweli kiongozi huyo wa upinzani anahitaji vitu hivyo.

“Huu ni msimu mwingine wa kuwakumbuka wasiokuwa nacho na maskini katika jamii. Tunathamini wale ambao wanatoa kuwapa watoto makao katika makao mbalimbali ya mayatima,” akaandika Rais Ruto kwenye mtandao wake wa kijamii.

“Niliwapa Krismasi watoto kutoka makao mbalimbali Uasin Gishu na maeneo jirani kwenye ikulu ndogo ya Eldoret,” akaongeza Rais.

Hata hivyo, mifuko hiyo kuandikwa ‘Rais William Ruto’ kisha kutundikwa picha ya kiongozi wa nchi kuliwakera baadhi ya watu mitandaoni wakisema hilo halikufaa.

“Ukitaka kuwapa msaada maskini fanya hivyo bila kupiga picha na kuweka picha yako katika mifuko ya misaada,” akasema Sam Aki Sam.

“Mnaiba asilimia 99 na kuwapa watu asilimia moja. Rais mbovu zaidi ulimwenguni,” akaandika Tosh Kipchumba.

Naye Bill Anyinga Wanyika akaandika, “Mnafikiria Wakenya hula Desemba pekee’

Wengi walimkemea Rais Ruto huku wakisema changamoto ambazo Wakenya wanapitia saa hii ni zaidi ya kujitangaza kuwa amewapa watoto mayatima misaada.

Wengi walimkumbusha kuhusu Bima Mpya ya Jamii, ufisadi na mwenendo wake wa kutoa ahadi za uongo kwa kuwa hajatimiza ahadi alizotoa kwa Wakenya kuelekea kura ya 2022.

Bw Oron ambaye anahudumu muhula wake wa kwanza bungeni kupitia ODM naye alionekana akimkabidhi Bw Odinga mbuzi watatu na kondoo watatu.

Alitoa zawadi hiyo nyumbani kwa Raila, Opoda, eneobunge la Bondo Kaunti ya Siaya.

Katika picha nyingine, alionekana akitoa bidhaa mbalimbali na vyakula kwa Mkewe Raila, Mama Idah Odinga.

Mbunge huyo ambaye anasemekana anamezea mate Ugavana wa Kisumu 2027 alikuwa ameandamana na Diwani wa Wadi ya Awasi/Onjiko Maurice Ngeta.

Wengi walijiuliza iwapo familia ya Raila ambayo ni tajiri kweli inahitaji zawadi hizo za Krismasi ama inastahili kuwaendea watu maskini.

“Kweli mwenye nacho ndiye huongezwa,” akaandika Evans Odhiambo Osambo.

“Hii ni kukosa fikira na kupeleka kitu kusikofaa,” akaandika Leonard Madanji.

Wanasiasa wengi hutumia zawadi kujivunia kura wakati wa kampeni na wengi walihusisha tukio la Bw Oron kama njia ya kusaka baraka za Raila amuidhinishe kama mwaniaji wa ugavana mnamo 2027.