Habari za Kitaifa

Ruto sasa arushia Kalonzo ndoano baada ya kuzomwa mkutano wa Linda Mwananchi

Na VITALIS KIMUTAI November 1st, 2026 Kusoma ni dakika: 2

KINARA wa chama cha Wiper Patriotic Front Kalonzo Musyoka anakabiliwa na mtihani mkubwa wa kisiasa huku Rais William Ruto akimshawishi kujiunga na serikali yake, wakati ambao washirika wake katika upinzani wanazidi kuwania tiketi kuuwakilisha katika uchaguzi wa urais wa 2027.

Kwa mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 73, uamuzi wa kuendelea na upinzani au kukubali ushirikiano na Rais Ruto unaweza kuamua hatima ya safari yake ya kisiasa ya takriban miaka 40.

Bw Kalonzo amekuwa akitamani kuongoza nchi tangu alipowania urais mara ya kwanza mwaka 2007. Baadaye alijitolea kumuunga mkono marehemu Raila Odinga katika chaguzi za 2013, 2017 na 2022, akiwa mgombeaji mwenza wake katika chaguzi mbili za kwanza.

Sasa, baada ya miaka mingi ya kumuunga mkono Raila, anataka nafasi ya kuongoza upinzani katika uchaguzi ujao. Hata hivyo, kuibuka kwa viongozi wapya kama Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na kinara wa Democracy for the Citizens Party (DCP) Rigathi Gachagua kumechanganya hesabu zake.

Bw Kalonzo na washirika wake walitaka suala la mgombeaji urais wa upinzani liamuliwe mapema, lakini Bw Sifuna na Bw Gachagua wanataka uamuzi huo uahirishwe wakisema kumtangaza mgombeaji sasa kunaweza kumpa Rais Ruto nafasi ya kugawanya upinzani.

Hali hiyo imemweka Kalonzo kwenye njia panda. Akibaki upinzani, anaweza kukosa tiketi ya urais. Akijiunga na serikali, hakuna hakikisho kwamba atapewa nafasi ya mgombeaji mwenza au wadhifa mwingine mkubwa.

Huku mjadala huo ukiendelea, viongozi wa serikali wameongeza juhudi za kumshawishi ajiunge na Rais Ruto.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen, Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot na msaidizi wa Rais Farouk Kibet Jumamosi walimhimiza Bw Kalonzo kuondoka upinzani.

Bw Murkomen alisema Kalonzo atakaribishwa serikalini na kwamba uzoefu wake wa kisiasa na kidiplomasia utathaminiwa.

Bw Cheruiyot, kwa upande wake, alidai viongozi wa upinzani hawana mpangilio wa kumshinda Rais Ruto mwaka 2027 na kumshauri Kalonzo ajiandae kwa uchaguzi wa 2032.

Bw Kibet alisema Kalonzo ataheshimiwa zaidi akijiunga na upande wa serikali.

Lakini washirika wa Kalonzo wanapinga madai hayo, wakisema Rais Ruto anamtambua kama tishio kubwa zaidi katika uchaguzi ujao.

Seneta wa Kitui Enoch Wambua alisema juhudi za kumshawishi Kalonzo ni ishara kwamba Rais anahofia uwezo wake wa kumshinda katika uchaguzi wa Agosti 10, 2027.

Alisema Kalonzo ana ushawishi mkubwa katika eneo la Ukambani, ambalo linaweza kuwa na wapiga kura2.2 milioni, kulingana na makadirio ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Wiper pia imesema haitaruhusu Kalonzo kuvurugwa na juhudi za kumshawishi ajiunge na serikali. Seneta wa Makueni Dan Maanzo alisema chama hicho kitaendelea na azma yake ya kuwania urais, akisema kuwa serikali jumuishi ni meli inayozama ambayo Kalonzo hapaswi kupanda.

Naibu Gavana wa Machakos Francis Mwangangi alisema Kalonzo anataka urais ili kuongoza taifa, na azma hiyo haihusishi kushirikiana na Rais Ruto.

Hata hivyo, mchambuzi wa siasa Profesa David Monda anasema Kalonzo anaweza kujiunga na serikali iwapo hatapewa tiketi ya upinzani.

Profesa Macharia Munene anasema upinzani unakabiliwa na ushindani wa maslahi binafsi, huku kila kiongozi akitaka kuongoza badala ya kujitolea kumuunga mkono mwingine.

Rais Ruto amekuwa akimshawishi Kalonzo kwa muda. Mnamo Mei 2025 alisema alimwendea kwanza baada ya uchaguzi wa 2022 kabla ya kumtafuta Raila, lakini Kalonzo akakataa pendekezo lake.

Wiki iliyopita, akiwa Tseikuru, nyumbani kwa Kalonzo, Rais alikosoa upinzani kwa kile alichokitaja kuwa kumdhalilisha kiongozi huyo, akimhimiza ajiunge naye badala ya kukabiliwa na mchujo mwingine wa kisiasa.

Hata hivyo, Kalonzo aliwahi kusema mwaka 2023 kuwa kuachana na azma yake ya urais kungeashiria kustaafu siasa.

Alisema alikuwa tayari kuwania urais mwaka 2002, 2013 na 2022, lakini alijitolea kuwaunga mkono wengine.