Makala

Wazee wazidisha juhudi kupatanisha Uhuru na Gachagua

Na MWANGI MUIRURI November 1st, 2026 Kusoma ni dakika: 3

JUHUDI mpya za kuunganisha Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha Democracy for the Citizens (DCP), Rigathi Gachagua, kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 zinaendelea kushika kasi, huku jina la Naibu Rais Kithure Kindiki likiibuka katika mpango huo.

Hii ni mara ya nne tangu 2022 ambapo viongozi hao wawili, waliokuwa washirika wa karibu kabla ya kuwa mahasimu wa kisiasa, wanashinikizwa kuweka tofauti zao kando ili kuunganisha eneo la Mlima Kenya.

Kwa mujibu wa taarifa tulizopata, mkutano wa hivi karibuni ulipangwa kufanyika Jumanne lakini Bw Kenyatta hakupatikana.

Mlezi wa kitaifa wa baraza la wazee la Kiama Kia Ma, Bw Kung’u Muigai, alithibitisha kuwa maandalizi ya kuwakutanisha viongozi hao yanaendelea. Alisema wanataka pia Prof Kindiki kuhudhuria ili viongozi wakuu wa eneo hilo wajadili mustakabali wake wa kisiasa.

“Tunakaribia kufanikiwa. Tunawaomba muwe na subira,” alisema, akiongeza kuwa Bw Kenyatta ndiye atakayetoa tarehe ya mkutano huo.

Jaribio la kwanza lilifanyika 2022, wakati Bw Gachagua alipotakiwa kushirikiana na Bw Kenyatta, aliyekuwa rais wakati huo, kuunganisha Mlima Kenya nyuma ya mgombea mmoja wa urais. Hata hivyo, Bw Kenyatta aliunga mkono Raila Odinga wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, huku Bw Gachagua akiwa katika kambi ya William Ruto wa Kenya Kwanza.

Bw Gachagua alipuuza wito huo na akaungana na  Dkt Ruto kushinda  uchaguzi. Aliteuliwa naibu rais lakini akatimuliwa mamlakani Oktoba 2024.

Kabla ya kuingia katika siasa za uchaguzi mwaka 2017, Bw Gachagua alikuwa msaidizi binafsi wa Bw Kenyatta kwa miaka 20. Baadaye alichaguliwa kuwa mbunge wa Mathira na kupanda hadi wadhifa wa naibu rais.

Uhusiano wao ulizorota wakati wa kampeni na zaidi baada ya Bw Gachagua kuwa naibu rais. Aliongoza mashambulizi ya kisiasa dhidi ya biashara za familia ya Kenyatta na miradi yake ya urithi. Mzozo ulifikia kilele wakati shamba la Northlands la familia hiyo, Ruiru, lilipovamiwa, mifugo kuibwa na sehemu ya ardhi kuchomwa moto.

Bw Gachagua amewahi kuomba msamaha hadharani kwa familia ya Kenyatta kutokana na matukio hayo, lakini Rais huyo  mstaafu hajatoa msimamo wa wazi kuhusu uwezekano wa maridhiano.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Kikuyu, Bw Wachira Kiago, alisema juhudi za kuunganisha jamii ni endelevu. Alisema jaribio la pili lilikwama baada ya hisia kali kuibuka pande zote mbili, huku siasa za kumuondoa Bw Gachagua madarakani zikitatiza mazungumzo.

Jaribio la tatu lilifanyika baada ya kuondolewa kwake, wakati wazee walipoona haja ya kuzuia wapiga kura wa Mlima Kenya kugawanyika bila mwelekeo wa kisiasa. Hata hivyo, juhudi hizo zilikumbwa na changamoto baada ya Rais Ruto pia kuanzisha mazungumzo ya kumkaribia Bw Kenyatta.

Mnamo, Bw Gachagua alipuuza madai kuwa kulikuwa na mkutano uliopangwa kati yake na Bw Kenyatta. Katika mahojiano na KTN, alisema hajapanga wala kuomba mkutano huo, lakini hakufunga mlango wa uwezekano wa kukutana naye iwapo kutakuwa na haja.

Kauli hiyo ilijiri licha ya Bw Gachagua kutangaza Julai 11 kuwa analenga kukutana na Bw Kenyatta nyumbani kwake Ichaweri ili kumweleza matokeo ya mashauriano ya karibu miezi miwili aliyofanya katika makazi yake ya Wamunyoro. Alisema pia atatafuta ushauri na baraka zake kuelekea uchaguzi wa 2027.

Mchambuzi wa siasa Mixson Gitau alisema wapiga kura wanataka viongozi hao waweke kando majivuno yao na kuungana. Alisema tofauti zao zimezua mpasuko mkubwa miongoni mwa wafuasi wao, huku miungano mipya ikiendeleza mgawanyiko huo.

Kwa sasa, Bw Gachagua anaendeleza azma yake ya urais huku akijaribu kushawishi Kalonzo Musyoka na Edwin Sifuna kuungana katika upinzani. Wakati huo huo, anamchukulia Dkt Fred Matiang’i kama mradi wa kisiasa wa Bw Kenyatta unaolenga kudhoofisha ushawishi wake Mlima Kenya.

Jina la Prof Kindiki linaongeza uzito katika hesabu hizo. Naibu rais amewahi kumuomba aliyekuwa gavana wa Meru, Kiraitu Murungi, amsaidie kumfikia Bw Kenyatta ili aunganishe jamii. Katika hafla moja ya sekta ya maziwa Meru, Prof Kindiki alimuomba Bw Murungi kumshawishi Bw Kenyatta kusaidia kuunganisha jamii ili isije ikapoteza mwelekeo.

Bw Joseph Kaguthi, anayeongoza juhudi za kuwakutanisha wazee, wataalamu na viongozi wa dini, alisema ajenda inayopendekezwa ni kuafikiana kuhusu maslahi ya pamoja, ushirikiano na namna ya kuhakikisha kura za eneo hilo zina umuhimu. Alisema mkutano huo unapaswa kufanyika kabla ya Desemba.

Bw Muigai alisema mkutano huo pia utajadili nani atakuwa msemaji wa kisiasa wa Mlima Kenya. Alisema Bw Kenyatta anatambuliwa kama mshauri mkuu wa eneo hilo tangu alipostaafu, lakini sasa wanahitaji msemaji atakayewasilisha msimamo wa jamii.

Bw Bernard Njue wa mrengo wa kisiasa wa Kiama Kia Ma alisema Bw Kenyatta na Bw Gachagua lazima wapunguze misimamo yao mikali ili mazungumzo yafanikiwe.

Alisema Bw Kenyatta anapaswa kumsamehe Bw Gachagua, huku kiongozi huyo wa DCP akionyesha kuwa anaweza kumshirikisha rais huyo wa zamani katika mipango yake ya kisiasa.

“Wote wawili lazima watambue kuwa mgawanyiko wao wa sasa hautunufaishi kama jamii. Wasipoungana, tutawagawanya watu wetu,” alisema.

Wazee wanasema Mlima Kenya hauwezi kumudu kuingia katika uchaguzi wa 2027 ukiwa umegawanyika. Wanataka viongozi hao wakubaliane kuhusu mwelekeo wa kisiasa ili kura za eneo hilo ziwe na nguvu, badala ya kugawanyika katika makundi yanayoshindana.