Habari za Kitaifa

Sababu ya LSK kupinga kaunti kuzika miili 120 iliyorundikana mochari, ikishukiwa mingi ni ya Gen Z

Na SAM KIPLAGAT September 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

CHAMA cha Wanasheria Nchini (LSK) kimewasilisha kesi kortini kikitaka serikali ya Kaunti ya Nairobi izuiwe kuzika miili 120 iliyohifadhiwa katikaMochari ya jiji la Nairobi, iliyokuwa hadi itakapotambuliwa.

LSK imesema serikali ya kaunti ilichapisha notisi mwezi uliopita, Septemba 2024, kuhusu mpango wake wa kuizika miili hiyo bila kuwapa watu muda wa kutosha kuitambua.

Chama hicho kimesema hatua hiyo inatokana na nia mbaya ya kutaka kuficha maovu yaliyofanyiwa watu waliouawa ambao miili yao haijatwaliwa.

“Pande husika zikisubiri kusikizwa na uamuzi wa kesi hii, agizo litolewe kushurutisha washtakiwa kutekeleza mchakato wa uchunguzi wa DNA ili kutambua miili 120 iliyohifadhiwa katika Mochari ya Jiji la Nairobi,” LSK inasema kwenye kesi iliyowasilishwa katika Mahakama Kuu Jumatatu, Septemba 2, 2024.

LSK imesema idadi kubwa ya vijana waliuawa kwa kupigwa risasi na wengine bado hawajapatikana tangu maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha yaliyofanyika Juni 25, 2024.

Afisa Mkuu Mtendaji wa LSK, Florence Muturi, alisema waandamanaji wengi ambao ni vijana waliouawa Nairobi walipelekwa katika Mochari ya Jiji la Nairobi (awali City Mortuary).

Alisema familia kadhaa zimekuwa zikiwasaka wapendwa wao ambao wametoweka tangu maandamano yalipoanza.

“Huku watu wengi wakiendelea kusaka wapendwa wao ambao wametoweka tangu maandamano ya Gen Z yalipoanza, Mshtakiwa 1 na 6 (maafisa wa serikali) wamechapisha notisi kwenye gazeti lililotokea Agosti 21, 2024 wakifahamisha umma wananuia kuzika miili 120 iliyoachwa Nairobi City Funeral Home katika muda wa siku saba ikiwa haitatambuliwa,” alisema.