Habari za Kitaifa

Sababu ya majasusi wa Serikali kumwandama Gachagua

Na MWANGI MUIRURI November 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua sasa anasema serikali inamuandama na kuchunguza mienendo yake kwa sababu zisizojulikana huku duru za usalama zikieleza kuwa ni kawaida kwa watu wenye ushawishi kama yeye kupigwa darubini.

Katika chapisho la karibu usiku wa manane kwenye mitandao yake ya kijamii mnamo Jumatano, Bw Gachagua alisema “maajenti wa usalama katika magari yasiyo rasmi wamekuwa wakinifuata popote ninakoenda”.

Aliongeza: “Wanaegesha gari kwenye lango la makazi yangu ya Nairobi, wakichunguza wageni wangu wote, na wananifuata kila ninapotoka nyumbani, hata hadi nyumbani kwangu mashambani”.

Msemaji wa Huduma ya Polisi Dkt Resila Onyango hakujibu maswali yetu kutaka maoni kuhusu suala hilo.

Msemaji wa serikali Bw Isaac Mwaura pia hakupatikana kwenye simu na jumbe zilizotumwa kwenye simu yake kutaka maoni yake kuhusu usalama wa Bw Gachagua bado hazijajibiwa.

Hata hivyo, duru katika makao makuu ya polisi jijini Nairobi ziliambia Taifa Leo kwamba usalama unatolewa kwa njia nyingi.

“Inafahamika kwamba Bw Gachagua anasalia kuwa muhimu kwa uthabiti wa kitaifa. Ni mtu wa kututia wasiwasi sana hasa kutokana na hisia za kisiasa ambazo ameweza kujenga kwa manufaa yake,” akasema.

Mwezi mmoja baada ya kuondolewa madarakani na wiki tatu tangu Rais William Ruto amteue Prof Kithure Kindiki kujaza nafasi yake, Bw Gachagua amekuwa akitoa madai ya kutishwa na serikali.

Washirika wake, hasa katika maeneo ya chini ya Mlima Kenya na Nairobi wamekuwa wakiripoti visa vya kuandamwa na polisi, kutekwa nyara, mateso na wakati mwingine, kushambuliwa.

Mbunge wa Embakasi ya Kati Benjamin Gathiru ameripoti kuwa wengi wa wale wanaomuunga mkono Gachagua wanafuatiliwa na maafisa wa polisi wanaoendesha magari ya Subaru ambayo hayana nambari za usajili.

“Wanatuandama, hatuwezi hata kuwasiliana kwa amani, maafisa wamejipangia kazi ya kutufuatilia,” alisema.

Mnamo Oktoba 22, 2024 Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ilimtaka naibu rais wa zamani kwenda katika makao yake makuu katika Kaunti ya Kiambu ili kueleza zaidi madai ambayo alikuwa ametoa kuhusu serikali kutaka kumuua.

Baada ya kutoka katika hospitali ya Karen mnamo Oktoba 20, 2024 ambapo alikuwa amelazwa ghafla kwa siku tatu, Bw Gachagua alidai kuwa serikali ilijaribu kumuua mara kadhaa, ikiwa ni pamoja na alipokuwa hospitalini.

Bw Gachagua alisimulia visa alivyodai maafisa wa usalama wa serikali walijaribu kumuua mara mbili kabla ya kuondolewa afisini.

“Ninataka kuwaambia watu wa Kenya kwamba sijihisi salama na pia ninataka wajue kwamba ikiwa lolote litanipata  anayepaswa kulaumiwa ni Rais Ruto,” Gachagua alisema.

Alidai kuwa alipangwa kuuawa mnamo Agosti 30, 2024 alipoandamana na rais katika ziara eneo la Nyanza.

“Waliingia katika chumba changu, na mmoja wao akajaribu kutia sumu kwenye chakula changu, lakini tuligundua na kukwepa mpango huo,” Gachagua alidai.

Mwezi mmoja baadaye akiwa katika Kaunti ya Nyeri, Bw Gachagua alidai, maajenti wa serikali walijaribu kutia sumu kwenye chakula alichopaswa kula pamoja na ujumbe wa Baraza la Wazee wa Kikuyu.

Alisisitiza kwamba aliripoti matukio hayo mawili kwa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) ingawa malalamiko yote ya uhalifu yanapaswa kuripotiwa kwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi na kurekodiwa katijka Kitabu cha Matukio (OB).

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA