Habari za Kitaifa

Sababu za polisi kukatazwa kumzuilia mwanaharakati Mwangi

Na RICHARD MUNGUTI July 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MWANAHARAKATI Boniface Mwangi na wengine wanne waliokamatwa Alhamisi wakiandamana dhidi ya serikali wameachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu Sh20,000 kila mmoja.

Akiwaachilia huru, Hakimu Mkuu wa Milimani Gilbert Shikwe alimuonya Bw Mwangi na wenzake wanne kutoingilia uchunguzi.

Akikataa ombi la polisi la kuwazuilia Mwangi, Robert Otieno, Albert Wambugu, Pablo Chacha na Erot Franco kwa siku 21 hakimu huyo alisema makosa yanayochunguzwa ni madogo.

Shikwe alisema polisi wanaweza kuchunguza makosa, washukiwa wakiwa nje kwa dhamana.

Aliwaagiza washukiwa hao kushirikiana na wapelelezi kabla ya kuagiza kesi hiyo itajwe Agosti 16 2024 kwa maagizo zaidi.

Hakimu alikubaliana na mawakili wa utetezi kwamba dhamana ni haki ya kikatiba.

“Dhamana ni haki ya kikatiba kwa washukiwa ambao wako chini ya uchunguzi wa polisi,” Shikwe aliamua.

Pia alisema hakuna sababu za msingi za kuitaka mahakama kuwanyima dhamana washukiwa hao.