Habari za Kitaifa

Sababu za serikali ya Sakaja kulipa wakili Sh1.3 bilioni

Na  Joseph Wangui April 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Wakili mashuhuri jijini Nairobi, Donald Kipkorir, yuko mbioni kupokea Sh1.3 bilioni kutoka kwa serikali ya Kaunti ya Nairobi kama malipo kwa huduma zake za kisheria katika kesi mbili zilizohusiana na umiliki wa ardhi ya jeshi na uhalali wa kanuni za huduma ya zimamoto jijini.

Hii ni baada ya Jaji wa Mahakama Kuu, John Chigiti, kuamuru serikali ya kaunti inayoongozwa na Gavana Johnson Sakaja kumlipa wakili huyo kupitia kampuni yake ya sheria, KTK Advocates, kiasi hicho ndani ya siku 60 pamoja na riba.

Amri hizo zilizotolewa Aprili 3 zinalenga serikali ya kaunti, waziri wa fedha wa kaunti, afisa mkuu wa fedha na wakili mkuu wa kaunti.

Jaji Chigiti alisema hakuna sababu ya msingi iliyotolewa kuchelewesha malipo hayo, na iwapo mahakama ingeepuka kutoa amri za kulazimisha malipo hayo, basi kampuni hiyo ya sheria isingekuwa na njia yoyote ya kupata haki licha ya kuwa na amri halali za malipo.

Alitoa amri hizo kufuatia ombi la kampuni ya Bw Kipkorir, ambayo ilidai kuwa serikali ya kaunti ilikataa kulipa ada za huduma za kisheria za jumla ya Sh1,338,709,459 bila sababu yoyote.