Salasya amtaka Ruto kumuajiri awe mshauri wake
MBUNGE wa Mumias Mashariki, Peter Salasya amemtaka Rais William Ruto kuwaondoa kwenye orodha yake ya marafiki baadhi ya wanasiasa na washauri anaodai wanamhadaa kiongozi wa nchi.
Akizungumza Jumatatu, Januari 20, 2025 katika hafla ya Ruto eneo la Mumias, Kakamega, kuzindua mpango wa marupurupu ya wakulima wa miwa, akiwataja kama ‘makateli’ Bw Salasya alisema wanasiasa hao wanapotosha Rais.
Mbunge huyo machachari na jasiri, alimwambia Rais Ruto kwamba mabroka hao wanamdanganya kuwa mambo ni shwari chini ya utawala wake ila mambo nyanjani ni tofauti kabisa.
Salasya alisema Wakenya kutozwa ushuru (VAT) wa juu, akitumia mfano wa mshahara wa wafanyakazi kuvamiwa na kutozwa ada mara dufu, ni ishara kuwa wananchi wanaumia.
Mbunge huyo, vilevile alitaja bima tata ya afya ya SHIF, kama pendekezo ambalo Rais amepotoshwa na wanaomzingira kama washauri.
“Rais ninajua wewe una moyo wa kusaidia Kenya, lakini una makateli wanaokuzingira. Wanakudanganya kwamba SHA inafanya kazi, lakini haifanyi,” Bw Salasya alisema.
Akizua utani, mbunge huyo alimhimiza Rais Ruto ‘kumteua’ kama mshauri wake.
Salasya, aidha, alisema chini ya ushauri wake, Rais Ruto atashuhudia mabadiliko ya uongozi na Wakenya wataanza kumshabikia.
“Hao makateli wanaokuzingira walikudanganya ukafinya Mkenya kwenye mshahara wake kwa kuwakelea makato. Tafadhali Rais, niajiri kama mshauri wako na nitakuambia ukweli,” alielezea.
Bw Salasya, hata hivyo, alimmiminia sifa kiongozi wa nchi akisema hatua ya kuwapa wakulima wa miwa bonasi ni ya kwanza kuwahi kushuhudiwa Kenya na ya kihistoria.
Uongozi wa Rais Ruto umekuwa ukikosolewa, hasa kufuatia kupanda kwa gharama ya maisha kutokana na mapendekezo ya kuongeza ada na VAT kwa bidhaa muhimu za kimsingi.
Mwaka uliopita, 2024, taifa lilishuhudia maandamano yaliyoendeshwa na Gen Z wakilalamikia kupanda kwa gharama ya maisha na kukosa ajira.
Vijana hao walipinga kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2024, ambao baadaye Rais Ruto aliufutilia mbali kufuatia presha.
Maandamano hayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 60.
Baadhi ya vipengele vya mswada huo tata, vinaonekana kutekelezwa kisiri – kupitia machapisho ya mara kwa mara kwenye Gazeti Rasmi la Kiserikali.