Habari za Kitaifa

Sasa ni miereka ya sera katika siasa — si vyama, Wachanganuzi wasema

Na JUSTUS OCHIENG January 8th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

KAMPENI za urais nchini zinaanza kuchukua sura mapema, mwaka moja kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027, huku 2026 ukiibuka kama wa kushawishi wapiga kura, wagombeaji wakijaribu kunadi sera zao kwa wananchi.

Mwaka mmoja tu kabla ya Uchaguzi Mkuu, ushindani hauko tu kwa nani anayegombea, bali ni kile anachopanga kufanya na kama wapiga kura wataamini ahadi hizo zinaweza kuwanasua kutoka mzigo wa ushuru mkubwa, gharama ya maisha inayoendelea kuongezeka, deni linaloongezeka na kuwafanya warejeshe imani kwa taasisi za umma.

Rais wa sasa William Ruto anajitetea kwa ajenda yake ya maendeleo yenye malengo makubwa, huku wapinzani wakiahidi kuimarisha uchumi na kuongoza kwa maadili.

Mashindano haya yanaibuka kama kura ya maamuzi kuhusu utawala, mtindo wa uongozi na mustakabali wa taifa.

Mpango wa Ruto umejikita katika nguzo nne: upatikanaji wa elimu; kubadilisha Kenya kuwa nchi ya kujitosheleza kwa chakula, kuongeza megawati 10,000 za umeme ndani ya miaka saba; na kuendesha mradi mkubwa wa miundombinu unaojumuisha kupanua kilomita 28,000 za barabara na barabara kuu 2,500.

Kwa Rais Ruto, uchaguzi wa 2027 unahusu uendelevu dhidi ya mabadiliko. Anawaomba wapiga kura kuamini maono yake makubwa ya muda mrefu, akisisitiza kuwa maumivu ya mageuzi leo yatazalisha ustawi kesho.

Lakini anakabiliana na upinzani kutoka kwa vyama mbalimbali.Upinzani unaungana, ukileta pamoja washirika wa zamani wa Ruto, wanasiasa wenye uzoefu wa miaka mingi, wataalamu na wanaharakati.

Miongoni mwa wakosoaji wakuu ni aliyekuwa mwanasheria mkuu na kiongozi wa Democratic Party, Justin Muturi, ambaye sasa ni kinara wa Muungano wa Upinzani. Muturi anashutumu Rais Ruto kwa kuvamia taasisi za utawala na kudhoofisha mfumo wa ukaguzi.

“Tumebaki na Mkaguzi Mkuu, Mdhibiti wa Bajeti na kwa kiwango kikubwa Mahakama,” alisema.

Alimshutumu Rais Ruto kwa kupuuza njia za kimsingi za mipango na bajeti, akisema “Anaamka na kutangaza Sh1.4 bilioni kwa Uwanja wa Bukhungu. Pesa hizo zilipangwa wapi? Nani alikubali?”

Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, ambaye uhusiano wake na Rais Ruto umeathiri pakubwa siasa nchini, anajitambulisha kama kiongozi wa mageuzi.

Ameahidi kurudisha elimu bila malipo ya kweli, huduma za afya, na kuondoa kodi za nyumba zinazolemaza wananchi.

Kiongozi wa Wiper Patriotic Front Bw Kalonzo Musyoka amekita kampeni yake katika kuondoa Rais Ruto madarakani, kuondoa ushuru anaosema umelemea Wakenya na kuwafanya maskini na kupigana na ufisadi.

Anaahidi kwamba, utawala wake utavutia wawekezaji kuunda nafasi za ajira na kupiga vita ufisadi. huku akiendeleza ujumbe wa umoja. Kalonzo ameweka macho yake kwa vijana ambao anasema wamepuuzwa na serikali ya sasa.

Naibu Kiongozi wa chama cha Jubilee, Fred Matiang’i, anajitokeza kama mgombea makini, akilenga kurejesha uadilifu, kurekebisha uchumi na kuwekeza katika wafanyakazi huku Martha Karua wa Peoples Liberation Party akisema muhula wa miaka mitano unatosha kuweka Kenya katika njia thabiti. Anajiwasilisha kama mtetezi wa maadili na haki.

Kiongozi wa chama cha Safina Jimi Wanjigi naye anatoa mapendekezo makali ya uchumi, akipendekeza ukaguzi wa deni na kupunguza ushuru huku Eugene Wamalwa wa DAP-K akijitambulisha kama atakayeleta mabadiliko katika utawala.

Peter Munya wa chama cha Party of National Unity (PNU) anasisitiza kuimarisha ugatuzi na uwekezaji katika kilimo na viwanda.

Wanaharakati kama Boniface Mwangi wanasema watamaliza ufisadi na ukosefu wa haki nchini, huku Okiya Omtatah akilenga kurekebisha mfumo wa urais wenye nguvu.

Jaji Mkuu mstaafu David Maraga anajiwasilisha kama mlinzi wa katiba na sheria.

Mchambuzi wa siasa Prof Gitile Naituli anasema upinzani mara nyingi unashindwa si kwa kukosa kura nyingi, bali kwa ukosefu wa mipango na mshikamano.