Habari za Kitaifa

Serikali haina pesa za kuwalipa, Duale aambia wauguzi wanaogoma

Na MANASE OTSIALO May 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAZIRI wa Afya Aden Duale Jumamosi alisema serikali haina pesa za kuwapa ajira ya kudumu wahudumu wa afya 8,500 ambao wamekuwa wakiandamana katika afisi yake.

Badala yake, Bw Duale aliwataka wawaandame magavana na Bunge la Kitaifa na Seneti kuhusu masaibu yao.

“Naomba mnisikize nyie wauguzi, nina Sh3.5 bilioni pekee za ajira ya mkataba ambao mnayo kwa sasa,” akasema akiwa Garissa.

Bw Duale alisema alishangaa kuwaona wauguzi hao wakigoma nje ya afisi yake ilhali katiba inasema wazi kuwa wanastahili kulipwa na kaunti.

“Kama wewe ni muuguzi na ulitia saini mkataba na kaunti, basi utalipwa na kaunti yako kufikia Julai 1, 2025. Natuma orodha ya malipo ya wauguzi kwa kaunti zote,” akaongeza.

“Ni gavana ndiye atajua iwapo umekuwa ukifanya kazi au la. Sasa nitajua aje kile kinachoendelea kwenye kaunti yako kama nimekaa jumba la Afya?” akauliza. 

Zaidi ya wahudumu 8,500 ambao waliajiriwa kwa kandarasi chini ya Mpango wa Afya bora kwa wote (UHC) wamekuwa wakiandamana wakitaka wapewe ajira ya kudumu na pensheni.

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna alikuwa amemtaka Bw Duale apate suluhu ya kudumu kwa malalamishi na maandamano hayo ya wauguzi.

“Bw Duale, tafadhali tafuteni njia ya kusuluhisha utata huu wa wahudumu wa afya waliokuwa chini ya mpango wa UHC ambao wanataka ajira ya kudumu,” akasema Bw Sifuna.

Kwa mujibu wa katibu huyo wa ODM, serikali ya kitaifa ina pesa za kutosha kuwaajiri wauguzi na wahudumu wengine wa afya.

“Hawa wahudumu wa afya wanajali maslahi yao,” akaongeza akisema amekuwa akipokea simu na jumbe kutoka kwa wahudumu wa afya hasa wauguzi ambao wanaandamana kutaka kupewa ajira ya kudumu.

Hata hivyo, Bw Duale amekuwa akisisitiza kwamba, wauguzi hao wanafaa waandame bunge la kitaifa na seneti ili wizara yake iongezewe mgao ndipo apate pesa za kuwaajiri.

“Viongozi wenu waende Seneti na Bunge la Kitaifa kuuliza pesa zaidi ili mpate ajira ya kudumu,” alisema.