Habari za Kitaifa

Serikali kubana matumizi kwa kuandaa hafla zake katika taasisi za umma

Na MARY WANGARI August 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MKUU wa Utumishi wa Umma Felix Koskei amesema serikali inalenga kuwajibikia Wakenya kifedha kwa kuandaa mikutano na warsha zake kwenye taasisi za serikali.

Bw Koskei amesema uamuzi huo umeafikiwa ili kubana matumizi ya pesa za serikali na kuelekeza rasilimali za taifa kwenye miradi ya maendeleo wala hakuna ubadhirifu katika matumizi ya pesa za serikalini.

“Kama serikali, tutaendelea kuhakikisha kila shilingi inayokusanywa kutoka kwa Wakenya walipa ushuru inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Tutahakikisha hakuna ubadhirifu na kuwepo matumizi bora ya raslimali,” akasema Bw Koskei.

Alikuwa akiongea jana katika Chuo cha Mafunzo ya Wanajeshi Kenya mjini Karen Nairobi katika hafla ya utoaji mafunzo kwa mawaziri 19 ambao waliapishwa Alhamisi wiki jana katika ikulu ya Nairobi.

“Mikakati ya kupunguza matumizi ya fedha ilianza zamani. Tuliteua mahala hapa kwa sababu ni asasi ya serikali, ni karibu na Nairobi na kwa sababu ni mazingira tulivu tunamoweza kuendesha shuguli yetu ya kutoa mafunzo bila kutatizwa,” akaongeza Bw Koskei.

Hapo awali ambapo mafunzo hayo kwa mawaziri yalikuwa yakifanyika katika hoteli za kifahari hususan mjini Naivasha.

Mkuu huyo wa watumishi wa umma alifafanua kuwa mafunzo hayo yanadhamiriwa kuwapa maarifa mawaziri wapya  ujuzi wa kutekeleza majukumu yao, hususan kwa wanaojiunga kwa mara ya kwanza na baraza la mawaziri.

Bw Koskei alisema mafunzo hayo yanakusudiwa kuhakikisha uwajibikaji na kuzuia ubadhirifu wa raslimali za umma kwa kuhakikisha, “kila waziri na katibu wa wizara yuko mstari wa mbele kupiga vita ufisadi katika wizara na idara wanazoongoza mtawalia.”

“Tunataka kuona vita vikali dhidi ya ufisadi. Kuhakikisha utekelezaji wa miradi kote nchini unaendeshwa kwa njia inayoridhisha pasipo ubadhirifu wowote,” alisema.

Kuhusu mtindo wa mawaziri kujishaua kwa maisha ya kifahari ikiwemo mavazi, Mkuu wa watumishi wa umma alisema baraza jipya litapatia kipaumbele “huduma kwa Wakenya.”

“Tunataka kuona huduma inayojikita kwenye mfumo ambapo kila afisa wa serikali kuanzia waziri hadi mtu wa ngazi ya chini kabisa katika wizara, anatilia maanani zaidi kuhudumia wananchi. Tunataka mabadiliko kamili. Badala ya kuwa mabosi wanakuwa watumishi wa watu na hivyo ndivyo tunataka kuhakikisha tangu mwanzo.”

“Masuala ya maisha ya kifahari, majigambo kwa kujilimbikizia vinono, ni jambo ambalo tumekubaliana litazikwa katika kaburi la sahau. Tujishughulishe sasa na utowaji huduma kwa Wakenya,”

Mkuu huyo wa watumishi wa umma alifafanua kuwa mafunzo hayo yanadhamiriwa kuwapa maarifa mawaziri wapya  ujuzi wa kutekeleza majukumu yao, hususan kwa wanaojiunga kwa mara ya kwanza na baraza la mawaziri.

Alisema kuwa Rais Ruto alishiriki kikao mapema Jumatatu na mawaziri wapya ambapo aliwapa “maagizo na ushauri thabiti kuhusu kinachotarajiwa kutoka kwao wanapoanza kazi.”

“Hatuna muda wa kutosha. Mawaziri waliotangulia walikuwa wamefanya kazi nzuri kwa kiwango fulani na hatutaki kasi hiyo ishuke. Tunataka hata utekelezaji wa kasi zaidi wa miradi. Rais aliwaeleza wazi kabisa, wajiandae upesi, wafanye kazi kwa karibu na makatibu wa wizara na kuhakikisha Wakenya wamehakikishiwa utowaji huduma.”

Mawaziri wapya wanatazamiwa kujifunza masuala kadhaa ikiwemo, kufahamishwa kuhusu wajibu wa baraza, hasa kwa wanaohudumu kama mawaziri kwa mara ya kwanza, kujuzwa kuhusu miradi inayondelea, mifumo ya oparesheni za serikali na wajibu wanaopaswa kutekeleza.

“Kwa mawaziri wapya, tunawapa mafunzo ili wafahamu kanuni za utumishi wa umma, wajibu wa baraza na jukumu la waziri binafsi, wanapoendesha shughuli zao katika afisi zao mtawalia.”

“Mafunzo haya yatawawezesha kuelewa serikali, kukutana, kushikamana na kuwa kikosi kimoja kitakachofanikisha ajenda aliyozindua Rais na kuwaahidi Wakenya.