Habari za Kitaifa

Serikali mbioni kuondoa hitaji la IEBC kupeperusha matokeo ya uchaguzi moja kwa moja

Na DAVID MWERE November 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haitalazimishwa kupeperusha moja kwa moja matokeo ya uchaguzi wa urais yanapotangazwa na Maafisa Wasimamizi katika vituo vya kupigia kura ikiwa mswada uliowasilishwa katika Seneti utapitishwa.

Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Uchaguzi wa 2024 unalenga kuondoa sehemu ya 39 ya Sheria ya Uchaguzi na kuanzisha nyingine, isiyohitaji IEBC kupeperusha matokeo ya uchaguzi huo pindi yanavyotangazwa vituoni.

“Sehemu hiyo mpya imeondoa hitaji kuwa IEBC ihakikishe matokeo yanapeperushwa kutoka vituo vya kupigia kura ili kuwezesha umma kuwa na ufahamu,” mswada huo unasema.

Kwa sasa IEBC inahitajika kupeperusha moja kwa moja matokeo ya uchaguzi kupitia skrini kubwa iliyotundikiwa katika kituo cha kitaifa cha kujumuisha kura, yanavyotangazwa katika vituo vya kupigia kura.

Ni kwenye skrini hizo ambapo vyombo vya habari huchukua hesabu hizo na kupeperusha kupitia majukwaa mbalimbali kuwezesha umma kujua mgombeaji anayeongoza, kwa kura ngapi na kutoka vituo vipi vya kupigia kura.

Sehemu mpya inayopendekezwa kwenye mswada huo inapendekeza kwamba matokeo yatakayotangazwa katika vituoni ndiyo yatakuwa ya mwisho.

Aidha, inasema kuwa kura za urais zitajumuishwa, kutangazwa na kutangazwa na kupeperushwa kieletroniki kabla ya matokeo ya nyadhifa zingine zote.

Mswada huo unaodhaminiwa kwa pamoja na Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot (Seneta wa Kericho) na mwenzake wa upande wa wachache Stewart Madzayo (Kilifi), ni zao la Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano (NADCO).

Kamati hiyo ilishirikisha wanachama kutoka muungano tawala wa Kenya Kwanza na ule wa Azimio la Umoja One Kenya.

Ilibuniwa na serikali kufuatia maandamano ya wafuasi wa upinzani baada ya Rais William Ruto kutangazwa mshindi katika uchaguzi wa urais wa Agosti 9, 2022.

IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA