Habari za Kitaifa

Serikali ya Kenya yaungama kukamata raia wa Uturuki kwa maagizo ya taifa hilo

Na CHARLES WASONGA October 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

HATIMAYE serikali ya Kenya imejitokeza na kuungama kukamata na kurejesha kwao raia wanne wa Uturuki walioripotiwa kutekwa nyara Ijumaa jijini Nairobi.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Katibu wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni Korir Sing’oei Jumatatu alisema hatua hiyo ilichukuliwa kufuatia ombi la taifa hilo.

Alisema kuwa haki za wanne hao zitalindwa kulingana na uhakikisho kutoka kwa serikali ya Uturuki.

“Serikali ya Kenya ilikubali ombi hilo kwa misingi ya uhusiano wa kihistoria na kimasilahi kati yake na Uturuki. Uhusiano uliohimiliwa katika mikataba kati ya nchini zetu,” akaeleza.

Dkt Sing’oei alikuwa mwepesi kuelezea kujitolea kwa Kenya kulinda na kuendeleza haki za wakimbizi inavyohitajika kwa mujibu wa sheria za kitaifa na zile za kimataifa.

“Kenya inazingatia usiri wa watu waliorejeshwa makwao na haijibu maswali kutoka kwa wanahabari kuhusu suala hilo hadi uchunguzi unaoendeshwa na asasi mbalimbali utakapokamilika,” akaeleza.

Raia wa Uturuki waliotekwa na watu wasiojulikana ni; Mustafa Genç, mwanawe wa kiume Abdullah Genç, Hüseyin Yeşilsu, Necdet Seyitoğlu, Öztürk Uzun, Alparslan Taşçı, na mkewe Saadet Taşçı.

Hata hivyo, iliripotiwa kuwa Abdullah Genç, Necdet Seyitoğlu, na Saadet Taşçı waliachiliwa saa chache baada ya kutekwa.

Lakini Öztürk Uzun, Alparslan Taşçı na Hüseyin Yeşilsu hawakuachiliwa.

Watu hao waliingia nchini Kenya kama wakimbizi wakihofia maisha yao nchini mwao.

Duru zilisema kuwa wakimbizi hao ni wanachama cha vuguvugu la kidini kwa jina, Gülen movement.

Wanachama wa vuguvugu hilo wamekuwa wakiwindwa na serikali ya Rais Recep Tayyip Erdoğan tangu kufeli kwa jaribio la mapinduzi ya serikali yake 2016.

Inasemekana kuwa wanachama wa Gülen movement ni miongoni mwa waliohusika kupanga mapinduzi hayo.