• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:55 AM
Serikali yaondoa hofu ya mlipuko wa Covid-19

Serikali yaondoa hofu ya mlipuko wa Covid-19

NA WANDERI KAMAU

WIZARA ya Afya imepuuzilia mbali hofu kwamba ongezeko la maradhi ya kupumua nchini limetokana na urejeo la maradhi ya Covid-19.

Kwenye taarifa mnamo Alhamisi, wizara ilitaja hali hiyo kuchangiwa na mafua ya kawaida.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Afya, Dkt Patrick Amoth, alisema kuwa visa vya mafua huwa vinaongezeka sana kati ya Februari na Machi, na Julai hadi Novemba.

Hata hivyo, alisema kuwa wanafuatilia uwezekano wowote wa kurejea kwa virusi vipya vya ugonjwa wa Covid-19 aina ya JNI, tangu Novemba 2023.

Alisema wizara imekuwa ikifuatilia visa hivyo kwa kubuni mfumo maalum wa kubaini uwepo wake. Alisema mfumo huo umekuwa ukitumika kwa miongo miwili iliyopita.

Dkt Amoth alisema kuwa ongezeko la visa vya watu wanaosumbuliwa na mafua huwa inashuhudiwa katika wakati huu wa mwaka, akipuuza hofu yoyote kutokana na idadi ya watu ambao wamelazwa hospitalini; au maafa ambayo yameshuhudiwa kutokana na mafua hayo.

“Hakuna visa vyovyote vya Covid-19 ambavyo vimeripotiwa. Kile kimeripotiwa ni ongezeko la visa vya mafua ya kawaida,” akasema.

Hata hivyo, aliwaagiza wananchi kuchukua tahadhari kwa kuepuka kutangamana na watu wanaoonyesha dalili za maradhi ya kupumua, kupata chanjo dhidi ya aina za mafua, kutumia barakoa katika maeneo ya umma na kuosha mikono kwa sabuni.

Alisema kuwa mafua hayo huwa si makali, kwani Wakenya wanaweza kujitibu bila kuenda hospitalini.

Hata hivyo, yanaweza kusababisha vifo katika baadhi ya watu wenye matatizo ya kiafya.

Taarifa hiyo inajiri wiki moja baada ya madaktari nchini kuelezea hofu kuhusu ongezeko la maradhi ya kupumua nchini.

Baadhi ya wataalamu wamehusisha hali hiyo na urejeo wa virusi vya Covid-19.

  • Tags

You can share this post!

Elimu: Taita Taveta yakabiliwa na uhaba wa walimu, mimba za...

AMINI USIAMINI: Kuku ni ‘mjukuu’ wa T-Rex

T L