Habari za Kitaifa

SHIF yaandamwa na dosari za kushangaza ikianza kazi Oktoba mosi

Na DANIEL OGETTA October 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

BIMA mpya ya Mamlaka ya Afya ya Kijamii (SHA) inaanza kazi leo Oktoba mosi, huku Wakenya waliojisajili wakikatizwa tamaa na kero la data ambazo zimesheheni makosa tele.

Wakenya sasa wanatarajiwa kukatwa asilimia 2.75 ya mapato yao kwa SHA yenye malengo ya kufanikisha huduma sawa za afya kwa wote.

SHA imechukua nafasi ya Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) kwa lengo la kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kupitia nyongeza ya makato ya kila mwezi.

Mfumo huu mpya utasimamia hazina tatu kuu ikiwemo Hazina ya Afya ya Jamii (PHI), Bima ya Afya ya Jamii (SHIF) na Hazina ya Dharura na Maradhi Sugu.

Huku SHA ikichukua usukani rasmi, Collins Otieno ni miongoni mwa Wakenya wanaohisi mambo yanakwenda mrama huku akikabiliwa na matatizo kuhusiana na dosari katika data aliyotumia kujisajili hali ambayo imemwacha na maswali tele.

Collins alijiandikisha na SHA siku tano kabla ya uzinduzi ili kuepuka harakati za mwisho mwisho za kujisajili.

“Nilifungua akaunti ya SHA wiki moja iliyopita. Sikuongeza jamaa yeyote. Siku chache baadaye nilipoingia katika akaunti yangu nilikuta msichana wa miaka 11 ameongezwa,” alieleza Taifa Leo kwa mshangao.

“Binti huyu alipokuwa akizaliwa 2013, nilikuwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika chuo kikuu nikijitahidi kufuatilia masomo yangu. Sikuwa na wazo lolote kuhusu kupata mtoto,” alisema.

“Nilipofungua akaunti, nilichagua “nimeoa” lakini sikujaza jamaa yeyote anayenitegemea. Siku mbili baadaye, niligundua maelezo hayo yasiyo ya kawaida. Nilijaribu kubadilisha lakini hakukuwa na namna ya kufuta.”

Kama mtaalamu wa teknolojia, Collins anafahamu vyema kuhusu mitambo lakini kitendawili hiki kimemshinda kutegua.

“Afisa wetu anayesimamia wafanyakazi alipendekeza nikague akaunti yangu ya NHIF na hakukuwa na jamaa mle. Mfumo mpya umevurugwa hata kabla ya kuanza kutekelezwa,” akaongeza

Waziri wa Afya, Deborah Barasa alithibitisha kwamba, kufikia Jumatatu, Wakenya wasiopungua  milioni 2.16  walikuwa tayari wamejiandikisha na SHA kabla ya kuzinduliwa rasmi.

Collins ni miongoni mwa Wakenya kadhaa wanaoripoti kuhusu dosari kuhusu maelezo yao wasijue la kufanya.

Kwa wengine kama Abiya Ochola, siyo mara ya kwanza kukumbana na kero hilo huku akisimulia yaliyompata kupitia NHIF.

“Nilikumbana na suala hili katika NHIF. Nilipooa, niliamua kuongeza maelezo yangu ambapo niligundua nilikuwa na mke na watoto watatu ambao sikuwafahamu! Ilibidi nihusishe wakili ili kutatua kero hilo,”

Virginiah alipojiandikisha na SHA, alishtuka kugundua ana mapacha barobaro ilhali kitindamimba wake anaelekea kuhitimu umri wa miaka 30.

“Baada ya kujisajili, nilikuta nina mapacha wenye umri wa miaka 14. Kitindamimba wangu anahitimu miaka 30 siku chache zijazo,” anaeleza.

Kwa upande wake Margaret Kagiri, tatizo ni kwamba jamaa wake wote wanaomtegemea hawaonekani kwenye akaunti yake.